Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameonya kwamba mzozo unaoongezeka kati ya Iran na Israel unafikia haraka "hatua ya kutorekebishika tena", huku Washington ikitafakari uwezekano wa kuingia vitani.
"Kwa bahati mbaya, mauaji ya halaiki yanayotelekezwa na Israel huko Gaza na mzozo na Iran yanafikia haraka hatua ya kutorudi nyuma. Wazimu huu lazima ukomeshwe haraka iwezekanavyo," Erdogan alisema Ijumaa.
"Ni muhimu wachochezi wa vita wazuiliwe kabla ya uharibifu zaidi, umwagaji damu, vifo vya raia na maafa ya kutisha, ambayo yanaweza kuathiri ukanda wetu, pamoja na Ulaya na Asia kwa miaka ijayo," alisema.
Erdogan aliilaumu serikali ya Netanyahu kwa "mauaji ya halaiki" yanayotokea Gaza, akiwashutumu wale wanaokaa kimya mbele ya mauaji hayo kuwa washiriki katika uhalifu huo.
"Wale wanaoigeuza Gaza kuwa kambi kubwa zaidi ya mateso duniani na kisha kuzungumzia uhalifu wa kivita sio tu kwamba wanapingana, lakini wanaonyesha ukosefu wa aibu na ukosefu wa adabu," alisema.
Pia alitoa wito kwa mataifa yenye ushawishi juu ya Israel kuepuka kuhadaiwa " na mchezo wa Netanyahu" na badala yake kutumia uwezo wao kusaidia kuanzisha usitishaji vita na kurejesha utulivu katika eneo hilo.
"Pamoja na mbinu za vitisho za lobi ya Wazayuni dhidi yangu na serikali yangu, hatujawahi kuyumba katika msimamo wetu na hatujawahi kusita kuwaunga mkono wanaodhulumiwa," Erdogan alibainisha.
Uhamiaji, hatari za kuvuja kwa nyuklia
Matamshi yake yametolewa katika kongamano la vijana la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Istanbul kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa OIC mwishoni mwa juma.
Miongoni mwa waliotakiwa kuhudhuria ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, huku mzozo unaoendelea na Israel huenda ukaangaziwa katika ajenda katika mazungumzo hayo ya siku mbili.
Iran na Israel zimekuwa katika vita kwa siku nane baada ya Israel, kusema Iran iko karibu kupata silaha ya nyuklia na hivyo kuanzisha wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya mpinzani wake mkuu, na kusababisha jibu la mara moja kutoka Tehran.
Hapo awali Erdogan alionya kwamba vita hivyo vinaweza kusababisha ongezeko la uhamiaji katika mazungumzo ya simu na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz.
"Msururu wa ghasia zilizochochewa na mashambulizi ya Israel unaweza kudhuru eneo na Ulaya katika suala la uhamiaji na uwezekano wa kuvuja kwa nyuklia," alisema, akionya kwamba mzozo huo "umepandisha tishio kwa usalama wa kikanda kwa kiwango cha juu".
Licha ya mashambulizi ya mabomu yanayoendelea, chanzo cha wizara ya ulinzi ya Uturuki kilisema Alhamisi kuwa "hakuna ongezeko" la idadi ya watu wanaovuka mpaka wa nchi hiyo kutoka Iran.
Wakati wa ziara ya mpakani siku ya Jumatano, Waziri wa Ulinzi Yasar Guler alisema, "hatua za usalama katika mipaka yetu zimeongezwa".