Mambo muhimu ya kuzingatia kama uko katika mahusiano ya mbali
Mambo muhimu ya kuzingatia kama uko katika mahusiano ya mbali
Mawasiliano siku zote ndio kitu muhimu katika kuwaweka karibu wale walio katika mahusiano ya mbali.
18 Julai 2025

Baadhi ya marafiki, wenza na hata wapendanao mara nyingi wamekiri kwamba, kuendeleza mahusiano ya mbali imekuwa ni vigumu kwao, kwa sababu ya umbali uliopo kati yao.

Hii inachangiwa zaidi, kwa sababu watu wawili, aidha ni marafiki au hata wapenzi, wanapokuwa mbali, basi nguvu zaidi ya rasilimali ya muda inahitajika ili kuendeleza uhusiano huo.

Hata hivyo, ukizingatia yafuatayo, basi inaweza kusaidia kudumisha mapenzi yenu au hata urafiki uliopo kati yenu.

Mawasiliano
Mawasiliano siku zote ndio kitu muhimu katika kuwaweka karibu wale walio katika mahusiano. Tafiti nyingi zinaonyesha mahusiano mingi yamevunjika, kwa sababu tu, mawasiliano yalivunjika. Wabobezi wa mahusiano, wanakiri kwamba, mawasiliano ni sawa na mbolea shambani.

Mawasiliano yamekuwa mepesi hasa katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali.

Tofauti na miaka ya nyuma, ambayo watu walitegemea njia ya barua ambayo ilikuchukua muda mrefu, au simu za mezani, ambazo nazo zilikuwa na gharama kubwa, mawasiliano ya sasa yanategemea zaidi upatikanaji wa mtandao.

Hivyo, unaweza kutumia fursa zilizopo kuweka mahusiano yako karibu kupitia njia mbalimbali za mawasialiano.

Zawadi za mara kwa mara
Zawadi ni ishara ya upendo, lakini pia ni uthibitisho kwamba, mpenzi wako yuko salama na upo katika fikra zake. Haijalishi ni zawadi ya aina gani, inaweza kuwa kubwa au ndogo.
Jenga tabia ya kupeana zawadi wakati wowote unapopata fursa.

Ongeza ubunifu

Muda mwengine unatakiwa kuongeza ubunifu, na kutengeza kumbukumbu nzuri, hata kama uko mbali na mpenzi wako. Kwa mfano, unaweza kuamua kuandika barua kwa kutumia hati zako. Kuna hisia tofauti mtu anaposoma barua au ujumbe ulioandikwa kwa kutumia hati za mkono, tofauti na zile za kuchapisha.

Usichoke kumwambia unampenda
Unaweza kuona kama vile ni jambo la kawaida lililozoeleka, lakini ni vyema, kila unapopata fursa ya kuwasiliana na mpenzi wako aliye mbali, kumhakikishia kwamba unampenda. Hii inaleta faraja, hasa kwa wapenzi waliombali.

Tumia utani katika mazungumzo
Wakati mwengine, unaweza kujikuta huna cha maana cha kuzungumza na mpenzi wako, hii inaweza kusababishwa na vitu kadhaa ikiwemo uchovu wa siku, au hata kukosa mada maalaumu. Jaribu kuanzisha mazungumzo kwa kutumia utani. Mzaha siku zote unaongeza upendo na kuleta afya katika mahusiano.

Kubali kujishusha

Usiogope kufanya kinachoonekana kama mambo ya ‘kitoto’ kama vile kumrushia busu, yani ‘flying kiss’ au hata kutumia emoji mbalimbali zinazoashirika hisia zako.

Kuwa muwazi

Usiogope kuelezea hisia zako. Kama siku hiyo umeamka ukiwa umejaa njozi za mpenzi wako, basi usisite kumwambia. Hii inasaidia kuwaleta karibu zaidi.

Mjulishe ratiba yako ya siku

Ni vyema kila mmoja kujua ratiba ya mwenzie. Hii inasaidia kujua ni muda gani sahihi wa kuwasiliana hasa kwa kituo.

Kwa mfano, bila shaka mchana utakuwa katika mihangaiko ya majukumu ya kila siku, hivyo ni vyema mwenzio ajue, ili hata atakapokupigia au hata kukutumia ujumbe, ategemee kuwa unaweza kushindwa kujibu kwa wakati. Kufanya hivi itasaidia kuondoa dhana mbaya.

InayohusianaTRT Global - Hizi ni baadhi ya dalili kwamba umemvutia, lakini anakusubiri uchukue hatua

Weka mpango wa kukutana ana kwa ana

Baada ya muda mrefu wa kuwa mbalimbali, ni vyema kuwa na mpango wa kukutana, angalau mara moja kwa mwaka.

Hii inasaidia kumpa mtu matumaini kwamba hatimae kuna mpango wa kuonana.

 

 

 


CHANZO:TRT Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us