Afrika
2 dk kusoma
Trump akashifiwa baada ya kuikejeli nchi ya Lesotho
Lesotho imemjibu Rais wa Marekani Donald Trump baada ya rais huyo kusema hakuna mtu anayeijua nchi hiyo.
Trump akashifiwa baada ya kuikejeli nchi ya Lesotho
Raia wa Lesotho wameghabishwa na Trump kwa kuikejeli nchi yao.
tokea masaa 6

Nchi ya Lesotho imelaani matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump, baada ya rais huyo kusema kwamba ni nchi ya Kiafrika ambayo ‘’hakuna aliyewahi kusikia’’. Nchi hiyo imesema matamshi ya Trump yalikuwa ya matusi.

Trump aliitaja Lesotho katika hotuba yake katika Bunge la Marekani Jumanne jioni huku akiorodhesha baadhi ya matumizi ya kigeni aliyopunguza kuwa ni "ufujaji mbaya".

Alitaja mradi wa awali wa msaada wa dola milioni nane ‘’katika taifa la Afrika la Lesotho, ambalo hakuna mtu amewahi kulisikia.’’ Matamsho hayo yaliwachekesha wabunge waliokuwepo hapo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Lesotho Lejone Mpotjoane alisema alistaajabishwa na matamshi ya Trump, akamwalika rais huyo kutembelea nchi yake. Mpotjoane alisema matamshi hayo ni ya madharau.

"Nimeshtushwa sana kwamba nchi yangu inaweza kutajwa hivyo na mkuu wa nchi," aliiambia Reuters.

Lesotho ni nchi ya Kusini mwa Afrika inayojulikana kwa mandhari yake nzuri ya mlima na idadi ya watu wapatao milioni 2.

Ina milima yenye mwinuko wa juu na wastani na wakati mwingine huitwa kama Ufalme wa Angani.

"Lesotho ni nchi muhimu na ya kipekee duniani kote. Ningefurahi kumualika rais, pamoja na dunia nzima kuja Lesotho," alisema Mpotjoane.

Mpotjoane amemtaka Trump aseme yeye binafsi haijui nchi hiyo na sio kusema hakuna anayeijua Lesotho.

Ameongeza kusema ameshangazwa na kauli ya Trump, kwa sababu Marekani wana ubalozi wao katika nchi ya Lesotho.

Utawala wa Trump umepunguza mabilioni ya madola ya misaada ya kigeni duniani kote huku ukijaribu kuoanisha matumizi na sera ya Trump ya "Marekani Kwanza".

Mpotjoane alisema Lesotho inahisi athari ya kupunguzwa kwa misaada kwani sekta ya afya imekuwa ikitegemea msaada huo kwa muda, lakini serikali inaangalia jinsi ya kujitegemea zaidi.

"Lazima tukubali. Lakini kutaja nchi yangu hivyo, ni jambo la kushtusha," alisema Mpotjoane.

Hata hivyo mfanyabiashara na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa X, ameomba leseni ya miaka 10 ili kutoa huduma za intaneti Lesotho kupitia mfumo wa ‘Starlink’.

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us