Somalia imezindua kampeni ya chanjo ya nchi nzima siku ya Jumatatu kukabiliana na magonjwa ya suruwa au ukambi, polio, na nimonia ikilenga kufikia watoto zaidi ya milioni 3 kote nchini.
Shirika la Afya Duniani (WHO), likishirikiana na serikali kuu ya Somalia na serikali za majimbo limezindua kampeni ya wiki nzima ya chanjo, imesema katika taarifa kwa lengo la "kuwalinda watoto na jamii zilizo katika hali mbaya kutokana na magonjwa yanayoweza kukingwa" katika eneo hilo.
Shirika la Vaccine Alliance (GAVI) linafadhili kampeni hiyo, ambayo inalenga kuwapa chanjo watoto milioni 3.1 nchini Somalia wasiozidi umri wa miaka mitano dhidi ya suruwa au ukambi, polio, na nimonia, taarifa hiyo imesema.
Kwa muda sasa Somalia inakabiliwa na changamoto za kiusalama, kuifanya iwe vigumu kutoa chanjo kwa watoto walio katika mazingira mabaya, kwa mujibu wa WHO.
Tangu 2014, hakujakuwa na aliyepatikana na ugonjwa wa polio nchini Somalia,na bara zima la Afrika lilitangazwa kutokuwa na polio 2020.
Hata hivyo, WHO inasema kuwa miundombinu ya afya ya nchini humo yamesambaratishwa na mapigano, umaskini, na mabadiliko ya tabianchi, na tatizo la polio linaendelea kuwatatiza watoto.
Mwezi Aprili, Somalia ilianzisha mradi wa chanjo mbili muhimu kitaifa, zote zikilenga kuwakinga watoto dhidi ya nimonia na kuharisha.
Ilisema kuwa ushirikiano huu ni hatua kwa taifa kupunguza maambukizi ya suruwa, nimonia, na kuharisha, ambayo ndiyo sababu kuu ya magonjwa na vifo miongoni mwa watoto wa Somalia.