Galatasaray wamepata ubingwa wao wa 25 ikiwa wamebakisha mechi mbili kukamilisha msimu baada ya kuwafunga kayserispor mabao 3-0 siku ya Jumapili.
Ushindi huo uliwapa Galatasaray wigo wa alama nane kutoka kwa mahasimu wao wa Istanbul Fenerbahce, ambao hawajawahi kushinda ligi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Galatasaray sasa wataongeza nyota tano kwenye jezi zao, kila nyota moja inawakilisha mataji matano.
Vilabu hivyo viwili vya Istanbul vilikuwa vinapambana kutafuta ubingwa, na Galatasaray wana alama 89 huku Fenerbahce, ambao wamewafunga Eyupspor 2-0 Jumapili, wakiwa na alama 81. Samsunspor wako nafasi ya tatu wakiwa na alama 60 kufikia sasa.
Mabao ya Osimhen msimu huu
Mshambuliaji wa Nigeria Victor Osimhen alifunga goli la kwanza katika dakika ya 26 kisha winga wa Uturuki Baris Alper Yilmaz akaongeza la pili dakika tatu baadaye katika kipindi cha kwanza.
Golikipa Fernando Muslera aliongeza la tatu kupitia mkwaju wa penati kipindi cha pili, na kuwahakikishia Galatasaray ushindi wakiwa jijini Istanbul, huku mashabiki wakisherehekea kote nchini.
Galatasaray imefungwa mechi moja tu msimu huu kwenye ligi na timu ya Besiktas. Wamepata mabao 87 na kufungwa magoli 31.
Kwa matokeo hayo, Galatasaray wamefuzu kwa Ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Walipata usaidizi mkubwa wa kupata taji hilo kutokana na juhudi za Osimhen kuzifumania nyavu mara 25 tangu alipotuwa kwenye klabu hiyo kwa mkopo akitokea Napoli mwezi Septemba.