Kwa nini soka inachochea mzozo wa DRC na Rwanda?
Afrika
5 dk kusoma
Kwa nini soka inachochea mzozo wa DRC na Rwanda?Mgogoro wa Rwanda na DRC unatishia mchezo maarufu wa kabumbu, huku serikali ya DRC ikitoa wito kwa vilabu vikubwa kusitisha ushirikiano na kampeni ya "Visit Rwanda" kama njia ya kuonesha kutoridhishwa na madai ya nchi hiyo kuunga mkono waasi wa M23.
Serikali ya DRC inataka vilabu vikubwa vya soka visitishe ushirikiano wao na kampeni ya "Visit Rwanda". Picha: Visit Rwanda
3 Machi 2025

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inayokumbwa na vita imeeleza kutofurahia mienendo ya baadhi ya vilabu maarufu vya soka duniani – Arsenal, Bayern Munich na Paris Saint-Germain – kuhusu ushirikiano wao wa ufadhili na kampeni ya "Visit Rwanda".

Michezo haina uhusiano wowote na umwagikaji damu; lakini mchezo huu unaopendwa zaidi duniani sasa uko kwenye utata wa masuala ya maadili na kuzingatia hali mbaya ya binadamu kutokana na mashambulizi ya waasi wa M23 mashariki mwa DRC, ikiwemo miji muhimu ya Goma na Bukavu.

Utata huu unatokana na serikali ya DRC kuishtumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekuwa ikikanusha. Rwanda inadai kuwa jeshi la Congo lilishirikiana na wapiganaji wa Kihutu wanaolaumiwa kwa mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi 1994.

Madai haya yamesababisha wasiwasi wa kimataifa, huku ukosefu wa usalama katika kanda hiyo ukidhihirika na kuwepo na hofu ya athari mbaya zaidi hata nje ya kanda.

Katikati ya vurugu hizi kuna suala la ufadhili wa soka ambao huingizia vilabu vikubwa vya Ligi Kuu ya England, vya ligi ya Bundesliga ya Ujerumani na vile vya Ligi Kuu ya Ufaransa mapato ya mamilioni ya madola.

Wito kwa vilabu

Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Thérèse Kayikwamba Wagner, hivi majuzi aliziomba timu za Arsenal, Bayern Munich na PSG kufikiria upya kuhusu ufadhili wao wa biashara na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda kuhusu mradi wao wa "Visit Rwanda", akitaja mapato yanayotokana na makubaliano hayo kuwa "yana damu".

Kaulimbiu ya "Visit Rwanda" imekuwa kwenye jezi za Arsenal tangu 2018. PSG na Bayern Munich wakajiunga katika miaka iliyofuata. Arsenal iliahidiwa dola milioni 40 kwa zaidi ya miaka mitatu, kampeni hiyo iliingizia PSG dola kati ya milioni $8-10.

2023 Bayern ilitia saini mkataba wa miaka mitano wa ushirikiano na Rwanda kutangaza maendeleo ya mpira wa miguu na utalii.

Kile kilichoanza kama mradi mzuri wa kutangaza zaidi utalii barani Afrika kupitia umaarufu wa vilabu hivyo kote duniani sasa limekuwa jambo lenye utata.

Kampeni ya DRC dhidi ya uhusiano wa Rwanda na michezo duniani haijaishia tu kwenye soka.

Maafisa wa DRC wametoa wito kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa mchezo wa magari ya langalanga Formula One Stefano Domenicali, wakimtaka afikirie wazo la kuipa Kigali nafasi ya kuandaa moja wa mkondo wa Grand Prix kwa madai ya uhasama unaofanywa na wanajeshi wa Rwanda na kulazimisha watu zaidi ya 700,000 kuhama makazi yao mwanzoni mwa mwaka huu kwa sababu ya vurugu zinazotekelezwa na M23.

Wizara ya afya ya Congo inasema kuna miili karibu 3,000 ambayo ipo katika vyumba vya kuhifadhia maiti vya Goma baada ya mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wa M23.

Msimamo wa Rwanda

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo ametaja ukosefu huu wa usalama kuwa ni kutokana na kushindwa kuweka mambo sawa kwa serikali ya DRC ambayo anadai imeshindwa kutatua matatizo ya raia wake.

"Raia hawa wamekuwa wakikabiliwa na vurugu za kikabila zinazotekelezwa na FDLR (wapiganaji wenye uhusiano na watu wa jamii ya Wahutu). FDLR ni kundi lenye silaha ambalo limeorodheshwa kuwa la kigaidi na Marekani,'' Makolo ameiambia TRT Afrika.

''Kundi hilo lilianzishwa na wale waliotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi 1994 na wameapa kurejea Rwanda 'kumaliza kazi' ambayo walishindwa kukamilisha 1994. Rwanda haitokubali hilo kufanyika," anasema.

Makolo anasema kama kweli serikali ya Congo inachukulia jambo hili kwa uzito na inataka amani kwa watu wake na usalama wa kikanda, ingevunja kabisa kundi la FDLR, na hivyo wangelikuwa wanalinda watu wao na kuondoa tishio la Rwanda kwao.

Katika kuelekeza madai yao dhidi ya Rwanda, DRC imesema Rwanda inatumia M23 kupora madini ya nchi hiyo katika eneo hilo.

"Jeshi la Rwanda lilikwenda kinyume na makubaliano ya usitishwaji wa mapigano ambayo nilikuwa nimeafikiana na mwezangu wa Rwanda na badala yake wakashambulia kwa mabomu nyumba na hospitali huko Goma, na kusababisha vifo vya watu karibu 3,000, kulingana na Umoja wa Mataifa," Waziri wa Mambo ya Nje Wagner alieleza katika barua yake kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Formula One.

Rais wa Rwanda Paul Kagame alitangaza Disemba mwaka jana kuwa nchi yake itaomba kuandaa moja ya mikondo ya mashindano ya Formula One katika mji mkuu Kigali.

Ukakasi wa chanzo cha fedha

Kwa Kagame, kuandaa Formula One ni sehemu ya "mkakati mpana kwa nchi yake kutumia michezo katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa taifa lake, utalii, na kutambulika duniani".

Rwanda, inayojulikana kama nchi yenye milima elfu moja, inalenga kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa mwenyeji wa Formula One Grand Prix tangu 1993. Barua hiyo kutoka kwa serikali ya Congo inaeleza wasiwasi kuhusu chanzo cha fedha za Rwanda ambazo watatumia kuandaa Grand Prix.

"DRC inaamini uporaji wa madini haya ya damu na Rwanda inaingizia nchi hiyo mapato ya dola bilioni 1 kila mwaka kwenye uchumi wao," inasema ripoti ya Umoja wa Mataifa.

Makolo anadai kuwa ushirikiano wa Rwanda na michezo na kampeni ya "Visit Rwanda" inaleta furaha kwa mamilioni ya watu, mbali na upatikanaji wa ajira, kuvutia zaidi watalii na kuingiza mapato.

"Ni wakati sasa kwa watu wa Congo kufaidi kutokana na fursa hizi, lakini hili linawezekana tu iwapo serikali ya DRC itaacha kutesa na kunyanyasa sehemu ya watu wake na kuishambulia Rwanda na badala yake watoe huduma na maendeleo kwa watu wake," ameiambia TRT Afrika.

"Madai haya ni kujaribu kupoteza dira ya nani hasa anahusika na mzozo huu wa DRC."

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us