Afrika
2 dk kusoma
Umoja wa Ulaya watoa wito kwa Rwanda kuondoa wanajeshi wake DRC
Suluhu la mzozo wa Congo ni la kisiasa, si la kijeshi, anasema mwakilishi wa EU katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika
Umoja wa Ulaya watoa wito kwa Rwanda kuondoa wanajeshi wake DRC
Umoja wa Ulaya waitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake DRC.
5 Machi 2025

Mwakilishi maalum wa EU katika eneo la Maziwa Makuu ya Afrika, siku ya Jumatano aliishutumu Rwanda kwa kukosa kuheshimu ardhi ya Congo na akahimiza kupatikana suluhisho la kisiasa la mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Vikosi vya Rwanda viko katika ardhi ya Kongo na lazima virudi nyumbani. Rwanda lazima pia iache kutoa msaada wa kijeshi na wa vifaa kwa M23," mwakilishi wa EU Johan Borgstram alisema katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Congo Kinshasa.

"Suluhu la mzozo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo sio la kijeshi. Suluhu la kisiasa linahitajika," Borgstram alisema, akiongeza kuwa Rwanda na Kongo ni lazima zitatue mzozo kisiasa, hakuna njia nyingine.

"Nchi hizo mbili lazima zifanye kazi ili kuanzisha mkataba wa maelewano ndani ya mfumo wa michakato ya kikanda," alisema, akitoa wito kwa mashirika ya kikanda kusimamia mazungumzo.

Borgstram alisema alipokuwa Rwanda, Rais Paul Kagame alielezea wasiwasi wa usalama wa nchi yake na kuashiria kile alichokieleza kuwa ni ukosefu wa dhamira ya kisiasa ya serikali ya Kongo kuhalalisha uwepo wa wanajeshi wa Rwanda katika ardhi ya Congo.

Hata hivyo, mwakilishi huyo wa EU alisema msimamo wa umoja huo ni kwamba "kuingilia kwa Rwanda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni kutoheshimu eneo la nchi hiyo."

Kundi la M23 liliimarisha udhibiti wake wa eneo mashariki mwa Kongo mwezi Desemba, na kuteka miji mikuu ya majimbo ya Goma na Bukavu.

Congo na nchi nyingine zinaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo, madai ambayo Rwanda inakanusha.

M23 inasema inatetea maslahi ya Watutsi wachache wa Congo, ambao wanadai kuwa wanabaguliwa kutokana na uhusiano wao wa kikabila na jamii ya Watutsi wa Rwanda.

Ujerumani siku ya Jumanne iliungana na Marekani na Uingereza katika kuiwekea Rwanda vikwazo vya kifedha kutokana na mzozo huo.

Takriban watu 80,000 wamekimbia mapigano ya silaha mashariki mwa Congo na kuelekea katika nchi jirani, ikiwa ni pamoja na karibu watu 61,000 ambao wamewasili Burundi tangu Januari, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi.

CHANZO:AA
Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us