Watoto wapatao 375,000 katika eneo la Kivu Kaskazini ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekosa fursa ya masomo kutokana na machafuko yanayoendelea eneo hilo.
Kulingana na Shirika la Save the Children, asilimia 17 ya shule katika eneo hilo, zimefungwa kutokana na machafuko yanayosababishwa na kikundi cha M23.
“Hali ni mbaya sana,” amesema Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo nchini DRC, Greg Ramm.
Kulingana na Ramm, watoto hao wako katika hatari ya kutumikishwa na majeshi yenye silaha, wakati machafuko yakiendelea Mashariki mwa DRC.
"Watoto hao wananyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu huku mustakabali wao na nchi ya DRC ukiwa katika hali mbaya," Ramm aliongeza.
Kulingana na Save the Children, mahudhurio ya shule katika eneo la Kivu Kaskazini yameshuka kwa kiwango kikubwa kuanzia mwezi Januari, wakati ambapo wanafunzi milioni 1.3 walidahiliwa.