Mjadala kuhusu ufanisi wa vikwazo barani Afrika unaendelea huku Rwanda ikiwa nchi ya hivi punde zaidi barani humo kukumbwa na vikwazo vya kimataifa.
Ujerumani, Uingereza, Marekani na Canada zimeiwekea Rwanda vikwazo vya biashara huku zikihusisha nchi hiyo na mzozo unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Nchi hizo zimeishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23 lenye silaha ambalo limeteka baadhi ya maeneo ya Mashariki mwa DRC.
Rwanda inakanusha madai hayo ambayo pia yameungwa mkono na DRC yenyewe na Umoja wa Mataifa. Rwanda inasema vikwazo havitasuluhisha mzozo wa DRC.
"Hatua zilizotangazwa na Canada dhidi ya Rwanda hazitasuluhisha mzozo," Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ilisema baada ya Canada kuamua kwamba itasitisha ushikirikiano katika biashara na ufadhili kwa Rwanda kama sehemu ya vikwazo vyake.
Pia imeshtumu zaidi baadhi ya mataifa ya magharibi kuwa na historia ya ukoloni.
"Nchi kama Ujerumani zina dhima ya kihistoria ya kukosekana kwa hali ya utulivu inayotokea mara kwa mara katika eneo hili zinatakiwa kufahamu vyema kuliko kuegemea upande mmoja," Rwanda imesema.
Je, vikwazo vitamaliza mzozo wa DRC?
Mzozo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaendelea kusababisha wasiwasi huku M23 wakidhibiti mikoa ya Kivu Kusini na Kaskazini katika eneo la Mashariki mwa nchi.
Rwanda inaendelea kujitetea kuwa inawalinda watu wake dhidi ya uvamizi wa FDLR kundi lenye silaha ndani ya DRC ambalo linachukuliwa kuwa haramu na serikali ya Rwanda.
"Wanaposhinikiza kuwekewa vikwazo kwa Rwanda (rais wa DRC) kuona kwamba Rwanda inalengwa atakataa kushiriki katika mazungumzo yoyote," Waziri wa Masuala ya kikanda wa Rwanda James Kabarebe amesema.
Botsang Moiloa, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anaonya dhidi ya kile anachokiita “kulaumu bila kutumia njia ya kidiplomasia.
"Hali nchini DRC ina mitizamo mingi na ina mikono mingi inayohusika kutoka mikoa mbalimbali duniani," Moiloa anaeleza TRT.
"Ikiwa diplomasia haitatumika kuhusu hilo na kuanza kunyoosheana vidole wakati tunatakiwa kushiriki katika mijadala ya kutafuta suluhu kwa ajili ya amani, tatizo hilo hatulalitatua," anaongeza.
Mazungumzo yoyote kuhusu DRC ambayo yatawatenga M23 wakiitwa waasi au vuguvugu, ni jambo lisilowezekana kwa sasa, ni wadau katika ghasia hizi na hatuwezi kuwaweka kando," anaongeza.
Umoja wa Afrika unasema mazungumzo ndio suluhu pekee
Umoja wa Afrika unasema majadiliano kati ya Rwanda na DRC ndio suluhu pekee la mzozo nchini DRC.
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya kanda ya Kusini mwa Afrika, SADC ilifanya mkutano Februari 2025 ambao ulihudhuriwa na rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa DRC, uliosisitiza kuhusu DRC kuwa na mazungumzo na M23 ili kuondoa vikwazo vyovyote.
"Historia ya mzozo huo inajulikana sana na njia ya kusuluhisha ipo," Rais Yoweri Museveni amesema kwenye akaunti yake ya X.
"Tangu mwanzo ushauri wetu kwa pande zote zinazohusika serikali ya DRC - na kundi la M23 ulikuwa ni mazungumzo," aliongeza.