Rwanda imekashifu vikwazo vya Canada dhidi yao, huku nchi hiyo ikiihusisha Rwanda na kikundi cha M23 kinachofanya mashambulizi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokraisia ya Congo, DRC .
Canada haiwezi kudai kufurahishwa na juhudi za wahusika wa kikanda katika mchakato wa amani wakati inailaumu Rwanda kwa ukiukwaji wa mambo ya msingi, huku ikishindwa kuiwajibisha Serikali ya DRC, "wizara ya mambo ya nje ya Rwanda imesema katika taarifa.
Serikali ya Canada imetangaza kusitisha utoaji wa vibali vya uuzaji wa bidhaa maalum na teknolojia kwa taifa hilo.
Pia inasitisha makubaliano yoyote mapya ya biashara kati ya nchi hizo mbili, pamoja na kusimamisha ushirikiano wa biashara katika sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na kutoruhusu serikali au makampuni kutuma wajumbe kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Canada pia imesema haitashiriki katika hafla za kimataifa zinazoandaliwa nchini Rwanda.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imesema lawama hizo kutoka canada hazikubaliki na itatafuta ufafanuzi kuhusu hili kutoka kwa serikali hiyo.
Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda imesema vikwazo havitatatua changamoto ya usalama nchini DRC.
"Hatua dhidi ya Rwanda zilizotangazwa na Canada hazitasuluhisha mzozo huo. Rwanda itaendelea kufanya kazi na viongozi wa kanda katika mchakato uliokubaliwa wa upatanishi unaoongozwa na Waafrika, wakati tukiendelea kulinda usalama wa taifa letu ."
Serikali ya rais Kagame imesema Canada haiwezi kudai kuridhishwa na juhudi za wahusika wa kikanda katika mchakato wa amani, ilhali inawalimbikizia lawama Rwanda, na kushindwa kuiwajibisha Serikali ya DRC pia.
Rwanda tayari imewekewa vikwazo na Uingereza na Marekani huku Umoja wa Ulaya ukisema bado unatafakari suala hilo.
Mwezi Februari mwaka huu Rwanda ilisitisha uhusiano wake na Ubelgiji ikidai kuwa nchi hiyo iliamua kuegemea upande wa DRC katika suala hili.
Umoja wa Afrika na Jumuiya za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika zimeongeza juhudi za kutafuta suluhu kwa mvutano kati ta DRC na Rwanda na kusitisha mashambulizi ya M23. Hata hivyo bado M23 inaendelea kuwashambulia wakazi wa Mashariki mwa nchii hiyo ikiwa tayari imedhibiti Kivu kaskazini na Kivu Kusini.