Afrika
2 dk kusoma
Mahakama ya Uganda ina madeni ya kodi
Katibu wa Mahakama Uganda anasema Wizara ya Fedha haiwapi fedha za malipo ya kodi.
Mahakama ya Uganda ina madeni ya kodi
Mahakama Uganda inasema ina madeni ya kodi
4 Machi 2025

Katibu Mkuu wa Mahakama Uganda Pius Bigirimana, ametishia kuwaomba wamiliki wa nyumba kufunga majengo ya mahakama kutokana na Wizara ya Fedha kuendelea kutotoa fedha za malipo ya kodi.

Alifichua kuwa, wakati fulani, analazimika kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli nyingine za Mahakama ili kulipa malimbikizo ya kodi.

“Suluhisho mbadala ni kufunga ofisi na kuwatoa majaji. Itakuwa sijakiuka sheria; Nitafunga ofisi. Na kuna athari kwa hilo-kesi hazitaendelea," Bigirimana aliyasema hayo wakati alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) .

"Sio eti natishia. Nitawaambia wenye nyumba wafunge ofisi, na nitafanya hivyo kutoka hapa mbele yenu iwapo wabunge watasisitiza kuwa ninakiuka sheria, ”

Mahakama iliitwa kujibu hoja za ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2024, ambayo ilionesha kuwa zaidi ya dola laki 215 (shilingi milioni 790) zilitumika kulipa malimbikizo ya kodi licha ya kutokupangiwa bajeti kwa ajili ya hilo.

“Mahakama huendesha shughuli za mahakama kadhaa katika majengo ya kukodi. Licha ya gharama hizi za juu za uendeshaji, makadirio ya ufadhili wa zaidi ya laki 217 (shilingi milioni 800) kwa mwaka wa 2025/26 bado hayajafikiwa, na kusababisha kuzidi kwa malimbikizo. Uongozi inashirikisha Wizara ya Fedha kikamilifu ili kupata pesa zinazohitajika,” Stephen Naigo Emitu, Kamishna Msaidizi wa Fedha na Hesabu wa Mahakama alieleza.

Lakini wabunge kadhaa hawakukubaliana na maelezo haya wakidai kuwa inaonekana mahakama inafanya serikali kutumia fedha nyingi .

Gorreth Namugga mbunge wa Mawokota Kusini alibainisha kuwa malimbikizo ya deni la Mahakama yamefikia zaidi ya dola milioni 3.6 (shilingi bilioni 13.37).

“Hii inaonesha Mahakama inaiwekea serikali gharama bila kuwepo kwa bajeti hiyo. Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali alikuwa wazi kuwa sheria haikuzingatiwa,” Namugga alisema.

Katika kujibu, Mahakama iliwasilisha ushahidi wa maandishi kuonesha kwamba iliiandikia Wizara ya Fedha kuomba idhini ya kutenga fedha kwa ajili ya malipo ya kodi.

Hata hivyo hakuna majibu kutoka Wizara ya Fedha.

Katibu wa Mahakama, Bigirimana alilitaka Bunge lilazimishe Wizara ya Fedha kutoa maelezo ya kwa nini maombi ya Mahakama yanapuuzwa.

"Nadhani kinachotakiwa ni wizara ya fedha kuhojiwa. Tulikubaliana kwa mkataba kukodisha majengo ya mahakama kulingana na maelewano kwamba wizara hiyo itatoa pesa. Sasa, mnataka nifanye nini—niwaambie majaji waondoke katika majengo hayo? Hilo ndilo tatizo ninalokabiliana nalo,” alisema.

Alionya kwamba ikiwa mahitaji ya kodi ya Mahakama hayatotimizwa kikamilifu, malimbikizo yataendelea kuongezeka.

"Nawaahidi, hapa nitaendelea kuwa na malimbikizo ya kodi kwa sababu sina pesa," alisema.


Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us