Jordan imekataa hatua zozote zinazoweza kuhatarisha umoja wa Sudan, ikiwa ni pamoja na juhudi za kuunda "serikali mbadala," ambayo inaweza kutatiza kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo.
Taarifa iliyotolewa Jumapili na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imesema, msemaji wa wizara hiyo Sufian Qudah alithibitisha tena uungaji mkono wa Jordan kwa mipango inayohimiza utatuzi wa amani wa mgogoro wa Sudan sambamba na kulinda usalama wa nchi hiyo, uthabiti, mamlaka na ustawi wa watu wake.
Hapo awali, Misri na Saudi Arabia pia zilieleza kutofurahishwa na jaribio lolote la kuunda serikali mbadala ya Sudan.
Mnamo Februari 22, kundi la wapiganaji wa Sudan la RSF, pamoja na makundi ya kisiasa ya Sudan na makundi yenye silaha walitia saini mkataba wa kisiasa mjini Nairobi, Kenya kuunda serikali mbadala inayopinga mamlaka ya Sudan.
Serikali ya Sudan ilighadhabishwa na nchi ya Kenya kuruhusu mkutano huo ufanyike jijini Nairobi.
Mnamo Februari 20, Sudan ilimwita nyumbani balozi wake wa Nairobi, Kamal Jabara, kupinga hatua hiyo ya Kenya katika majadiliano yenye lengo la kuunda "serikali mbadala."
Hata hivyo Kenya ilitetea jukumu lake, ikisema kuwa kuandaa mikutano hiyo ni sehemu ya juhudi zake za kutafuta suluhu ya kumaliza vita nchini Sudan kwa uratibu wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Hapo awali nchi kama Saudi Arabia, Qatar na Kuwait zimepinga hatua ya kikundi cha RSF, kuunda serikali mbadala.