Uturuki inalenga kuimarisha uhusiano wake na Umoja wa Afrika wakati bara hilo likiadhimisha siku yake, Juni 25, 2025.
“Mwaka huu, tunaadhimisha miaka 20 ya nafasi ya Uturuki kama muangalizi ndani ya Umoja wa Afrika,” ilisema Wizara hiyo kupitia ukurasa wake wa X.
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje, Uturuki ni moja kati ya wadau wa kimkakati wa Umoja wa Afrika.
“Tunajiandaa kwa Mkutano wa IV unaohusisha ushirikiano kati ya Uturuki na Afrika, unaopangwa kufanyika mwaka 2026," taarifa hiyo ilisema.
Siku ya Jumapili, wizara hiyo ilitoa ujumbe maalumu kwenye tovuti yake, wa kuzipongeza nchi za Afrika kwa kuadhimisha siku yao.
“Siku ya Afrika huwakilisha matamanio ya watu wa Afrika ya kuwa na bara lenye umoja, amani, utulivu na ustawi pamoja na nia yao ya kuwa na nafasi katika mfumo wa kimataifa,” taarifa hiyo ilisema.
“Uturuki itaendelea kuwa mdau wa kweli na wa uhakika kwa nchi za Afrika, katika jitihada zao za kutimiza malengo hayo.”
Kulingana na taarifa hiyo, Uturuki ipo tayari kuendeleza jitihada za kukuza uhusiano wake na bara la Afrika kwa maslahi ya pande zote.
“Uturuki na Afrika zitaendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa mustakabali mmoja ambapo amani, utulivu na ustawi hutawala,” ilibainisha wizara hiyo.
Bara la Afrika limeadhimisha miaka 62 toka kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika.