Kiongozi wa AFC/M23 Corneille Nangaa amepongeza uamuzi wa Rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila wa kurudi nchini humo.
Kabila, ambaye anakabiliwa na tuhuma za uhaini kutokana na uhusiano wake na kikundi cha waasi wa M23, amerejea Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, akitokea Afrika Kusini.
Kulingana na Nangaa, Kabila amefanya maamuzi sahihi kuliko kuendelea kuishi uhamishoni.
“Tunapongeza ujio wake,” alisema kiongozi huyo wa AFC/M23 kupitia ukurasa wake wa X siku ya Jumatatu. “Amefanya maamuzi ya busara, haikuwa vyema kwake kuendelea kuishi uhamishoni.”
Ujio wa Kabila kwenye jiji la Goma, unakuja siku mbili baada ya kiongozi huyo wa zamani wa DRC kumtuhumu Rais Felix Tshisekedi kwa hadaa, dharau, ukabila, upendeleo na mambo mengine, ambayo, kulingana na Kabila, yamezorotesha umoja wa kitaifa.
Kabila, mwenye umri wa miaka 53, alikuwa kiongozi wa DRC kutoka mwaka 2001 hadi 2019, aliporithiwa na Tshisekedi.