Afrika
2 dk kusoma
Mfumo mpya Uganda wa usimamizi wa hakimiliki za wasanii
Sheria hiyo mpya pia itahakikisha wasanii wanalipwa kulingana na kazi zao na ina nia ya kukomesha uwizi wa haki za wasanii katika muziki.
Mfumo mpya Uganda wa usimamizi wa hakimiliki za wasanii
Rais wa Uganda Yoweri Museveni alikutana na viongozi wa wasanii . Picha/ Serikali ya Uganda
3 Machi 2025

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameidhinisha Mfumo wa Usimamizi wa Hakimiliki ili kuwalinda wanamuziki na kuhakikisha wanapata mapato kutokana na kazi zao.

"Sasa teknolojia inatakiwa kutuambia ni nani amecheza wimbo wa msanii na wapi," alisema Rais Museveni wakati wa mkutano na viongozi husika na wasanii katika eneo la Rwakitura magharibi mwa nchi.

Mfumo huu utawatetea wasanii kwani utahakikisha kazi za wanamuziki zinasajiliwa, utafuatilia matumizi ya muziki katika maeneo ya starehe, runinga na redio.

Sheria hiyo mpya pia itahakikisha wasanii wanalipwa kulingana na kazi zao na ina nia ya kukomesha uwizi wa haki za wasanii katika muziki.

Sheria itafanyaje kazi?

Sehemu kama vile maeneo ya starehe, vituo vya redio na TV vitahitaji kifaa chenye leseni ili kucheza muziki wa msanii wa Uganda.

Mfumo huo utafuatilia na kuhakikisha wanamuziki wanapata haki yao.

“Kwa mfano Ikiwa eneo la starehe linalipa Shilingi milioni moja kwa leseni ya muziki, wasanii watalipwa kulingana na mara ngapi muziki unachezwa. Wimbo uliochezwa mara 60 hupata 60% ya ada,” serikali ya Uganda imeeleza.

Maeneo ya starehe lazima yapate kifaa hiki ili kufuatilia nyimbo zilivyochezwa. Baraza la mawasiliano la Uganda lina jukumu la kufuatilia utekelezaji huu.

Serikali imesema Polisi wa Uganda watatekeleza sheria huku biashara ambazo hazitii sheria zikifungwa.

“Wanamuziki wengi wanatatizika kifedha baada ya miaka yao ya kuwa katika usanii kumalizika. Mfumo huu utahakikisha wanapata mapato ya kuwasaidia maishani kutokana na nyimbo zao, na kuwanufaisha pamoja na familia zao.” serikali imesema.

Maoni ya wananchi

Wasanii wamefurahia sheria hii kwani inawahakikishia kuwa na mapato wakati wote.

Hata hivyo wananchi wametoa maoni tofauti katika mtandao wa X.

“ Kutimiza hili huenda ikawa changamoto au haitawezekana hasa katika soko kama la Uganda ambapo nyimbo za Uganda zinashindana na zile kutoka Nigeria na Afrika Kusini ,” @digitalugandan amesema katika akaunti yake ya X.

Wananchi wengine wanasema gharama hii huenda ikawekwa kwa chakula na vinywaji vinavyouzwa katika maeneo ya starehe ambapo miziki hii huchezwa na hapo kuongeza bei ya bidhaa.

“Sasa natumai hata katika sekta ya filamu mabadiliko yatakuwepo. Televisheni zinazocheza filamu za bila malipo zinafanya vibaya. Zinafaa kulipia filamu za Uganda au kulipa zaidi kuonesha filamu za kigeni. Chaguo ni lao,” @agumemark_amesema.

Kuna wale ambao pia wanasema wale wasanii wachanga ambao hawajapata umaarufu bado huenda wakabaki nyuma kwani uwezekano wa makampuni kulipia muziki wao ni mdogo sana.





Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us