Bunge la Kenya limeeleza wasiwasi wake kuhusu wizara ya fedha kushindwa kutenga fedha katika makadirio ya bajeti ya 2025/26 kwa ajili ya maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika 2027.
Kamati ya bunge ya michezo na utamaduni nchini Kenya imeeleza wasiwasi wake kuhusu maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kutokana na ukosefu wa fedha.
Kama sehemu ya wajibu wake Kenya inahitaji kuwa na kiasi cha dola milioni 30 kufikia Aprili 2026.
Kenya imekumbwa na matatizo katika maandalizi yake ikiwa na upungufu wa fedha huku serikali ikijaribu kubana matumizi kutokana na kushindwa kukusanya kodi za kutosha.
Fainali hizo za 2027 zina wenyeji wenza ikiwa ni Kenya, Tanzania na Uganda. Fainali za wachezaji wa ligi za ndani barani (CHAN) ambazo zilikuwa zifanyike mwezi Februari 2025 ziliahirishwa hadi mwezi Agosti kutokana na miundombinu kutokuwa tayari. Katika mashindano hayo pia kuna wenyeji wenza ikiwemo Kenya, Uganda na Tanzania.
Kwa sasa hivi Kenya inaendelea na ukarabati wa baadhi ya viwanja, lakini fedha za maandalizi zilihitajika ili kukamilisha miradi hiyo pamoja na kulipa fedha za haki ya uwenyeji.
Serikali inasema kuna kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati, hivyo kukosekana pesa za kulipia haki za kuwa mwenyeji.