Ukifika Ethiopia jina la "Black Lion" au Tikur Anbessa kwa lugha ya Amharic, ni la kawaida.
Utaliona kwenye majengo mbalimbali ya serikali, vyombo vya usafiri, bidhaa mbalimbali, hata baadhi ya bendi za muziki zimejipa jina la mnyama huyo.
Kati ya mwaka 1935 na 1937, kitengo cha Jeshi la Ethiopia wakati wa Vita vya Pili kati ya Italia na Ethiopia kilifahamika kama ‘The Ethiopian Black Lions’. Na hii ndio sababu ya taifa la Ethiopia kujivunia kuwa nchi pekee barani Afrika kuwa na simba wa aina hii.
Simba mweusi, maarufu kama 'Simba wa Uhabeshi', anabakia kuwa mnyama wa kipekee na adimu barani Afrika.
Upekee wa simba hawa ni ‘masharubu’ yao mieusi, yenye kupamba shingo zao. Hii inatokana na mabadiliko ya kiasili.
Manyoya au masharubu hayo makubwa na mieusi huanzia kichwani na shingoni hadi kwenye sehemu ya tumbo, na huwa na umbo dogo wakilinganishwa na simba wengine.
Inaaminika kuwa, simba weusi wako katika hatari ya kutoweka, hasa kutokana na uchache wao kwa sasa.
Idadi ya sasa ya simba weusi nchini Ethiopia inakadiriwa kuwa chini ya 100. Pia, inaaminika kuwa simba wenye manyoya mieusi huvutia zaidi simba jike.
Wataalam wanasema simba dume wenye masharubu mieusi hutoa ‘vichochezi’ vya kiume vyenye kuhusishwa na uzalishaji wa mbegu za kiume zaidi, kuliko simba wenye manyoya ya kawaida.
Pia, manyoya yao makubwa na mieusi, huwasaidia wakati wa mapigano wakiwa poroni, yakiwatia hofu simba wengine kwani huwafanyaka waonekane kuwa wakubwa zaidi kwa umbo.
Vilevile, rangi zao nyeusi huwafanya wahisi joto zaidi kuliko simba wa kawaida, na hivyo simba hawa hupata changamoto zaidi wawapo mazingira ya joto, ukilinganisha na simba wengine, kwani joto hilo hufukuta ndani ya masharubu yao.
Simba wengine hata hupunguza ulaji wao wa chakula kwa sababu ya hali hii ya
joto na kuamua kuwinda muda wa usiku tu. Kwa Ethiopia, simba huyu atabakia kuwa hafari ya nchi hiyo kwa karne nyingi zijazo.
Alihusishwa na ishara ya ufalme wa Uhabeshi. Makaisari wengi walifuga
simba na hata Haile Selassie, aliyewahi kuiongoza Ethiopia kutoka mwaka 1930 hadi 1974, alipenda kuonekana akiongozana na simba weusi wawili wa kufugwa.
Hata wimbo wa mfalme wa reggae ulimwenguni, uitwao ‘Iron Lion Zion’ au ‘Simba wa Sayuni’, ulikuwa unamzunguzia simba huyo wa uhabeshi.
Hivyo basi, ukipata fursa ya kufika Ethiopia, tenga muda wako kwa kutembelea hifadhi za taifa za milima ya Simien na Bale, ule ujionee simba hawa wa kipekee.