AFRIKA
2 dk kusoma
Rais wa Msumbiji afanya mazungumzo na mpinzani wake huku kukiwa na wasiwasi
Taifa hilo la Kusini mwa Afrika limekumbwa na misukosuko ya kisiasa baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi uliozua utata. Katika uchaguzi Daniel Chapo alitangazwa mshindi wa kinyang'anyiro cha urais.
Rais wa Msumbiji afanya mazungumzo na mpinzani wake huku kukiwa na wasiwasi
Ushindi wa Daniel Chapo katika uchaguzi wa urais ulifuatwa na maandamano yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu. / AFP
24 Machi 2025

Rais wa Msumbiji Daniel Chapo amekutana na mwanasiasa wa upinzani Venancio Mondlane katika juhudi za kupunguza uhasama kufuatia miezi kadhaa ya makabiliano kati ya maafisa wa usalama na waandamanaji, ofisi ya rais ilisema Jumapili.

Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye utajiri wa gesi imekumbwa na ghasia za kisiasa tangu uchaguzi uliozua utata wa mwezi Oktoba.

Uchaguzi huo, ambao waangalizi wengi wa kimataifa walisema ulikuwa na dosari, ulifuatiwa na miezi miwili ya maandamano na vurugu na kusababisha vifo vya watu 360, kulingana na shirika mojawapo la kijamii la eneo hilo.

Chapo na Mondlane walikutana katika mji mkuu Maputo kujadili "suluhu ya matatizo yanayokabili nchi yao", ofisi ya rais ilisema katika taarifa.

‘Kuimarisha utulivu’

"Mkutano huu ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuhakikisha kuna utulivu na kusisitiza dhamira ya maridhiano," ilisema taarifa.

Haikufahamika moja kwa moja kama kuna makubaliano yoyote ya kisiasa yanayotarajiwa kwa Mondlane ambaye hivi karibuni alitengana na chama cha upinzani cha Podemos, ambacho kilimuunga mkono wakati akigombea urais.

Chapo aliapishwa mwezi Januari na mapema mwezi huu alitia saini makubaliano ya baada ya uchaguzi na vyama vingine tisa - ikiwemo chama cha zamani cha Mondlane cha Podemos.

Makubaliano hayo, ambayo yanasubiri kuidhinishwa na bunge, yanalenga kuanzisha mchakato wa marekebisho ya katiba.

Mondlane, ambaye ni maarufu miongoni mwa vijana, hakuhudhuria mazungumzo hayo, lakini alihamasisha mamia ya wanaomuunga mkono kufanya maandamano mjini Maputo.

Watu 14 walijeruhiwa katika makabiliano hayo na polisi.

Watu wasiopungua wawili waliuawa wiki iliyopita wakati polisi walipofyatua risasi katika maandamano yaliyohamasishwa na Mondlane.

Kuleta maridhiano

Majadiliano hayo ya kurejesha uhusiano ya Jumapili yanaonesha nia ya "kuleta maridhiano na kuimarisha majadiliano ya wazi yenye tija", ofisi ya rais ilisema, ikisambaza picha ya Chapo na Mondlane wakipeana mikono.

Hatua hii ya Chapo inakuja karibu wiki mbili baada ya Mondlane kusema kuwa amehojiwa kwa saa 10 na waendesha mashtaka na kuwekwa chini ya uangalizi wa mahakama.

Matokeo rasmi yanaonesha Mondlane alikuwa wa pili katika uchaguzi wa mwaka uliopita, na kumpa ushindi Chapo wa chama cha Frelimo ambacho kimekuwa uongozini tangu Msumbiji ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno 1975.

Chapo alipata asilimia 65, huku Mondlane akimaliza na asilimia 24.

Lakini kiongozi huyo wa upinzani anasema alishinda kwa asilimia 53, na aliungwa mkono kwa wingi kuwapa Frelimo ushindani wa kwanza wa kisawa sawa katika kipindi cha miaka hamsini.

CHANZO:AFP
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us