Serikali ya Trump inajiandaa kuanza kuwasafirisha wakimbizi kutoka Marekani hadi Libya, ambayo itakuwa hatua ya kuwapeleka wakimbizi wengi katika nchi ambayo iko kwenye vita kwa muda mrefu, shirika la habari la CBS lilitangaza siku ya Jumanne.
Maafisa wawili wa Marekani ambao wanafahamu kuhusu mipango hiyo wameiambia CBS News kuwa watu wataanza kusafirishwa kuanzia hata wiki hii and huenda hilo likatimizwa na jeshi la Marekani, katika kuendeleza mpango ambao tayari umeleta utata.
Kulingana na taarifa hiyo, haijulikani ni wakimbizi gani ambao watarejeshwa chini ya mpango huo unaopendekezwa au kama watachukuliwa na mamlaka za Libya watakapowasili.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa sasa imewaonya Wamarekani kuhusu kusafiri kwenda Libya, ikieleza hatari zilizoko ikiwemo "uhalifu, ugaidi, na mabomu ya ardhini ambayo hayajateguliwa, vurugu za watu, utekaji na mapigano."
Katika miezi ya hivi karibuni, Marekani imefanya mipango kwa wakimbizi kutoka bara la Asia na Afrika kupelekwa katika mataifa ya Marekani ya kati kama vile Costa Rica na Panama.
Ukosefu wa usalama Libya
Wanaume kadhaa kutoka Venezuela wanaodaiwa kujihusisha na magenge ya wahalifu walipelekwa nchini El Salvador, ambapo walipelekwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali zaidi.
Cha kushangaza, wanaume hao hawakupitia mchakato wa haki ili waweze kujitetea kuhusu madai ya kuhusika na magenge, huku marafiki zao wengi, jamaa zao, na mawakili wakilalamika kuwa walishtumiwa kimakosa.
Katika kesi ya Kilmar Abrego Garcia, 29, ambaye alikuwa kwenye ndoa na raia wa Marekani na alikuwa na hati ya mahakama inayozuia yeye kuondolewa nchini, serikali ya Trump inadai alipelekwa El Salvador kimakosa, lakini imekataa kuchukua hatua zozote za kumrejesha nchini, licha ya hukumu ya mahakama ya juu zaidi kutaka ifanyike hivyo.
Libya imekuwa kwenye mapigano tangu 2011, wakati kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi alipoondolewa madarakani baada ya kuwa uongozini kwa miongo minne.
Mwezi uliopita, Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Hanna Tetteh, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa raia wa Libya wanakabiliwa na matatizo katika maisha yao ya kila siku, ikiwemo matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa usalama, na hali tete ya kisiasa.
Alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kushirikiana katika kuwa na "mpango wa pamoja" kusaidia kuwepo kwa taifa la kidemokrasia ambalo litashughulikia masuala ya msingi ya watu wa Libya na kuimarisha uchumi wa nchi.