Katika misa yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa, 9 mei 2025 Papa Leo XIV alisema kuwa anatarajia kwamba kuchaguliwa kwake kunaweza kusaidia Kanisa Katoliki kuleta mwanga kwenye "usiku wa giza ulimwenguni".
Kadinali Robert Prevost , aliyechaguliwa Papa wa 267 wa Kanisa hilo 8 mei, 2025, alichagua jina la Leo XIV.
Papa mpya anapochaguliwa, moja ya mambo anayoyafanya rasmi kwanza ni kuchagua jina jipya.
Ni utamaduni ulioanza enzi za kati.
Si lazima kuchaguwa jina jipya lakini ni utamaduni uliokita mizizi.
Mara nyingi jina linaashiria dira ya Papa au muelekeo wake wa kiroho.
Jina lililochaguliwa mara nyingi ni ishara ya heshima kwa Mtakatifu muasisi wa jina hilo, Papa aliyetangulia, au urithi fulani ambao Papa mpya anataka kuiga.
“ Kupitia Huduma ya Petro, mmeniita niubebe msalaba huo na kubarikiwa na utume huo, na najua ninaweza kutegemea kila mmoja wenu kushirikiana nami tunapoendelea kama Kanisa, jumuiya ya marafiki wa Yesu, kama waumini, kutangaza habari njema, kutangaza Injili, “ Papa Leo XIV aliambia makadinali katika misa yake ya kwanza 9 Mei 2025.
Jina "Leo" lina umuhimu mkubwa wa kihistoria katika Kanisa Katoliki, likiwa limechaguliwa na Mapapa 13 waliotangulia kabla ya Leo XIV, na kulifanya kuwa mojawapo ya majina ya Papa yanayochaguliwa mara kwa mara.
Wataalamu wa masuala ya Kanisa Katoliki wanasema uchaguzi wa jina hili na Papa Leo XIV, unaweza kutafsiriwa kwa upana kama Prevost alitambua uwezo wa kihistoria wa Upapa kwa watangulizi wake waliokuwa na jina hilo la Leo, na pia kujitolea kwa haki kuhudumia kijamii ya sasa, akijipanga zaidi kufuata nyayo za Leo XIII.
Maelezo ya Kanisa ni kuwa kubadilisha jina kulianza karne ya sita na Papa John II, ambaye alibadilisha jina lake la kuzaliwa Mercurius kwa sababu lilihusishwa na mungu wa Kirumi.
Wakati huo, alihisi jina kama hilo halifai kwa kiongozi wa Kikristo. Tangu wakati huo, kila Papa amechagua jina alipendalo kuonesha dira yake ya Upapa.
Kwa nini Papa Francis hakuchagua jina ambalo limewahi kuchaguliwa?
Kadinali Jorge Mario Bergoglio alipotawazwa kuwa Papa, alichagua kujiita Fransisko baada ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, mtakatifu wa zama za kati aliyeanzisha Wafransisko, mojawapo ya daraja kubwa katika Kanisa Katoliki.
Papa Francis alichagua jina lake kwa heshima ya Mtakatifu Francis wa Assisi, akiashiria kuzingatia unyenyekevu, huduma kwa maskini, na utunzaji wa mazingira.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa jina hili kuchaguliwa na Papa yeyote.
“Alieleza hilo kwa njia rahisi sana, kwamba alichagua jina la Francis kwa sababu yeye ni mtu wa amani, kuhurumia maskini, na kuimarisha undugu. "Ni jina ambalo lina dira ya maisha," alielezea Kasisi Enzo Fortunato, ambaye aliishi Assisi kwa miaka 30.
Matarajio makubwa
Papa Leo XIV anaendelea kupongezwa na viongozi mbalimbali duniani, kila mmoja wao akieleza kuwa yuko tayari kufanya kazi naye.
Waumini katika sehemu tofauti duniani nao wametoa maoni yao kuhusu Kanisa kupata Papa mpya kutoka Marekani.
"Vyombo vya habari vilikuwa vimeionesha kwa namna ambayo Mmarekani hawezi kuwa Papa, kwa sababu Marekani ni mamlaka yenye uwezo mkubwa, ikimaanisha kwamba ukipata Papa kutoka Marekani, itakuwa kwamba Papa anatoka katika nchi ambayo tayari ina uwezo mkubwa duniani, basi ina maana kwamba tayari tumeshamuweka sawa Papa na Marekani. Hata hivyo, tunatakiwa kuelewa kwamba hii ni kazi ya Roho Mtakatifu, " padre Collings Quaidoo wa Ghana amesema.
“ Mungu amemchagua Papa, na tuna matumaini makubwa kwamba tutaendelea kufuata nyayo za Papa Francis,” Manuella Ganda Mona wa Ghana alisema.
"Kwa sababu yeye ni Mmarekani nadhani hiyo ni nzuri sana. Inatupa matumaini kwa hali ya kisiasa kuwa bora na kwa hali nzima ya kimataifa na kwa Kanisa pia kuimarika, " alisema Claudia Boelher, Mjerumani aliyekuwa kwenye ziara ya Vatican.
"Nimeshangaa kidogo. Hakuwa katika orodha ya wale waliokuwa wakizungumziwa. Nadhani itakuwa uwiano mzuri sana. Ila, nimesoma kidogo tu kumhusu hadi sasa, ni mchanganyiko mzuri sana wa Papa Francis na ulimwengu wote, kwa kweli, " Bernie Thomas ambaye ni padre amesema.
Raia wa Marekani wana maoni tofauti
Raia wa Marekani waliokuwa Vatican wakati wa tangazo la Papa mpya walitoa maoni tofauti .
“ Sikuwahi kutazamia kama Mmarekani angekuwa Papa hata katika kipindi cha miaka milioni moja kwa sababu tofauti, Trump akiwa uongozini na mambo mengine, Inaonekana kama Marekani itakuwa na uwezo mkubwa sana,”
“Na nadhani Wamarekani wengi ... siyo Wakatoliki, Wakatoliki ni wachache, hasa Wakatoliki wanaozungumza Kiingereza,” Lailah Brown, raia wa Marekani anasema.
“Na ninatumai pia, natarajia kuwa Marekani haitamuaibisha Papa mpya. Ni matumaini yangu kuwa Marekani itaanza kupunguza ubaguzi wa rangi.” ameongezea.
Lailah anasema kuwa anatarajia Papa kutoka Marekani kutaongeza waumini wa dini hiyo nchini humo.
“ Wahamiaji wengi wanaokuja Marekani ni Wakatoliki na wanaendeleza utamaduni huo. Lakini ni kama vile Mmarekani wa kawaida hashiriki katika Kanisa Katoliki, kama wao ni watu wa kufuata dini, wanakuwa katika Kanisa la Kiprotestanti. Kwa hivyo nimefurahi sana. Natumai Wamarekani wengi watajiunga na madhehebu ya Katoliki.
Wengine wanamuona kama aliyebeba matumaini ya amani ulimwenguni
"Natumai afanikiwe kuunganisha ulimwengu wote, kitu ambacho hatujafanya vizuri hivi karibuni kama Wamarekani." Jim Murray alisema.