Hali ya mshike mshike imeshuhudiwa katika mji wa Bukavu, nchini Congo, baada ya watu kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa huku milio ya risasi na milipuko ikitanda kwenye mkutano wa hadhara uliofanywa na kiongozi wa waasi wa M23, Corneille Nangaa. katika mji wa Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Alhamisi, wakaazi walisema.
Video imeonysha watu wakikimbia barabarani, wengine wakivuja damu huku wengine wakibeba miili iliyoko chini.
Wakazi walisema waliona maiti, lakini hakukuwa na taarifa za haraka kuhusu idadi ya waliopoteza maisha.
Nangaa ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kuwa rais wa Kongo Felix Tshisekedi aliamuru shambulio hilo, bila kutoa ushahidi. Hadi sasa hakuna taarifa yoyote kutoka kwa serikali ya Congo.
Nangaa alisema yeye na wanachama wakuu wa kundi la waasi wako salama.
Kundi hilo tayari limeteka maeneo mengi mashariki mwa nchi tangu mwanzoni mwa mwaka.
Kongo, Umoja wa Mataifa na mataifa yenye nguvu ya Magharibi yanasema nchi jirani ya Rwanda inaunga mkono kundi la waasi la Nangaa la M23 - tuhuma ambazo Rwanda inakanusha.
Kusonga mbele kwa waasi kumezusha hofu ya vita vya kikanda ambavyo vinaweza kushirikisha nchi jirani.
Katika hotuba yake kabla ya ufyatuaji risasi kuanza, Nangaa aliuambia umati wa maelfu ya watu kuwa M23 walikuwa wamekuja Bukavu kuleta usalama. Kundi hilo limedhibiti jiji hilo tangu Februari 16.
"Kutakuwa na vitengo maalum na doria ambazo zitafanyika katika jumuiya zote," alisema Nangaa, ambaye alikuwa akijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza Bukavu tangu kuchukuliwa kwa mamlaka hiyo.
Risasi ilianza mwishoni mwa mkutano, mkazi mmoja alisema. "Kulikuwa na ufyatuaji risasi kila upande. Hatujui kilichotokea. Kuna watu waliojeruhiwa, waliokufa, sijui."
M23 imekuwa ikijaribu kuonyesha kwamba inaweza kurejesha utulivu katika eneo ambalo imeteka kutoka kwa jeshi la Congo, na imefungua tena bandari na shule.