Nchini Kenya, mwanasheria aliyegeuka kuwa mwanaharakati na kuanza kupinga hali ilivyo nchini humo na kutafuta majibu kutoka serikalini.
Jina lake ni Morara Kebaso, ambaye sasa hivi amekuwa na ushawishi mkubwa katika upeo wa kisiasa.
Katika miezi ya hivi karibuni, sauti ya Morara Kebaso imekuwa ikisikika zaidi kwenye korido za siasa za Kenya.
Lengo lake ambalo ni la kijasiri, ni kuangazia jinsi miradi ya serikali inavyobuniwa, kutekelezwa, na kufuatiliwa, huku akiwakemea kupitia mitandao ya kijamii wanaotumia vibaya fedha za umma.
Safari ya Kebaso kuingia kwenye siasa ilichochewa na kuchoshwa kwake kama anavyosema mwenyewe, "Asilimia 70 ya watu niliosoma nao hawana chanzo cha mapato, na kwa sababu hiyo nimevunjika moyo kabisa na jinsi serikali imekuwa ikiendesha mipango na shughuli zake, jambo ambalo lilinichochea kuanza kutoa elimu ya uraia kwa umma kuelewa uzito wa hali hii na jinsi ilivyo hatari, ili waweze kufanya uamuzi wa kuleta mabadiliko. Kwa sababu unajua, viongozi wabaya hutokana na raia wabaya; ikiwa hatutaboresha ubora wa wananchi tulionao, hatutaboresha ubora wa uongozi tulionao."
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa vijana wanawakilisha karibu asilimia 84 ya raia wa Kenya wasio na ajira. Kwa hivyo, ujumbe wa Morara umewagusa sana raia waliokata tamaa.
"Morara anafanya kazi nzuri, na amefichua mambo ambayo hatukuyajua. Nina uhakika Wakenya wanafurahi, na ikiwezekana, anapaswa kuendelea vivyo hivyo," anasema Simon Mwangi, dereva wa bodaboda nchini Kenya.
Nae Wilson Kimanongo ambae ni mwalimu anaongeza, "Ikiwa humjui Kebaso, basi hauishi nchini humu."
Lakini harakati za Kebaso pia zimeibua ukosoaji. Katika mtandao wa kijamii wa X, baadhi ya watu wameelezea upinzani mkali, wakimtuhumu kwa kutafuta umaarufu kupitia siasa.
Hivi karibuni, mamlaka ilimkamata kwa muda mfupi, ikidai kuwa alihatarisha ‘amani ya umma,’ hatua ambayo baadhi waliiona kama jaribio la kumnyamazisha kutokana na wito wake wa utawala bora.
Serikali haikujibu ombi la TRT la kutaka kufanya mahojiano ili kujibu baadhi ya tuhuma hizo za ufisadi.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi inakadiria kuwa Kenya inapoteza takriban asilimia nane ya Pato Lake la Taifa, au karibu ya dola bilioni tano za Kimarekani kila mwaka, kwa ufisadi, udanganyifu, na usimamizi mbaya katika sekta muhimu kama vile miundombinu, huduma za afya na elimu.
Na Kenya inashikilia nafasi ya 126 kati ya 180 katika ripoti ya 2023 ya ‘’Transparency International’’ (Shirikia la Uwazi la Kimataifa) kuhusu viwango vya ufisadi.