Kipindi cha kwanza cha urais wa Denis Sassou Nguesso kilikuwa kati ya mwaka 1979 hadi 1992 na baadaye kurejea tena madarakani kuanzia mwaka 1997 na mpaka kufikia sasa ndiye rais wa taifa hilo la Afrika ya Kati.
Sassou Nguesso alizaliwa 1943 na alikuwa afisa wa jeshi ambapo alijiunga na jeshi 1960 muda mfupi kabla Jamhuri ya Congo kupata uhuru wake.
Baadaye alikuwa mkuu wa idara ya ujasusi jeshini. Katika miaka ya sitini alishiriki kwenye mapinduzi ya kijeshi nchini humo. Aliwahi kuwa waziri wa ulinzi akiwa na umri wa miaka 32.
Akiwa na chama chake cha PCT alishinda uchaguzi mkuu wa 1979. Akashinda tena uchaguzi wa 1984 na baada ya miaka mitano akarejea tena Ikulu kupitia uchaguzi wa 1989.
Alianzisha mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1990. Akashindwa kwenye uchaguzi wa 1992.
Alirejea nchini kutoka uhamishoni Januari 1997 na akashiriki uchaguzi wa mwezi Julai na kufikia mwezi Oktoba mwaka huo akaapishwa kuwa rais wa Congo-Brazzaville.
Nchi hiyo imekuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na makubaliano mbalimbali ya amani yamesainiwa pia.
Kufikia mwaka 2002 uchaguzi wa urais Sassou Nguesso alishinda kwa asilimia 89.41.
Baadhi ya waangalizi walidai uchaguzi haukuwa huru na haki.
Lakini alichaguliwa baada ya miaka mitano na mitano tena licha ya wakati mwingine upinzani kususia uchaguzi.
Mwaka 2009 alisema kuwa kuchaguliwa kwake mara kwa mara ni ishara ya ari ya kuendeleza ‘’amani, uthabiti na usalama.’’
Ukomo wa umri katika kugombea uliondolewa mwaka 2015, kwa taifa hilo lenye watu zaidi ya milioni sita.
Uchaguzi mwingine wa urais nchini Jamhuri ya Congo unatarajiwa kufanyika mwakani na haifahamiki kama Denis Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 81 atatetea nafasi yake au la.