AFRIKA
1 dk kusoma
Mkenya Stephen Munyakho, aliyeachiliwa kutoka gereza la Saudia arudi Kenya
Stephen Abdulkareem Munyakho, alinusurika kuuawa baada ya kukaa jela miaka 14 Saudi Arabia kwa kosa la mauaji.
Mkenya Stephen Munyakho, aliyeachiliwa kutoka gereza la Saudia arudi Kenya
Awali kuuawa kwa Stephen Munyakho kuliratibiwa Mei 2024 lakini kuahirishwa mara mbili kufuatia mchakato wa kidiplomasia wa Kenya. / Others
29 Julai 2025

Mkenya Stephen Abdulkareem Munyakho, ambaye amekuwa gerezani nchini Saudi Arabia kwa takriban miaka 14 amerudi nyumbani, baada ya kunusurika kuuawa kwa kosa la mauaji.

Munyakho alipatikana na hatia ya kumuua mfanyakazi mwenzake raia wa Yemen kwa kumchoma kwa kisu, baada ya ugomvi ofisini.

Awali mahakama ilimkuta na hatia ya mauaji bila kukusudia, kutokana na kuwa mfanyakazi mwenzake alimshambulia wa kwanza.

hata hivyo familia ya jamaa huyo kutoka Yemen ilikata rufaa ambapo mahakama ilibatilisha hukumu ya awali na kupatikana na hatia ya mauaji.

Malipo ya Diyya - ‘Fidia kwa damu’

Awali kuuawa kwake kuliratibiwa Mei 2024 lakini kuahirishwa mara mbili kufuatia mchakato wa kidiplomasia wa serikali ya Kenya.

Saudi Arabia inayotumia sheria ya Kiislamu, inaruhusu aliyepatikana na hatia ya mauaji kuachiliwa huru iwapo familia ya muathiriwa itakubali kupokea fidia kwa damu, inayojulikana kama ‘Diyya’.

Kuachiliwa kwa Munyakho kuliwezekana baada ya familia ya marehemu kukubali diyya ya dola milioni 1, na kuahirisha hukumu ya kifo iliyotolewa 2024.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Nje nchini Kenya, Waziri Mkuu Musalia Mudavadi alitoa shukrani kwa wote walioshiriki katika kuhakikisha uhuru wa Munyakho.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us