AFRIKA
2 dk kusoma
Rais wa Rwanda amteua waziri mkuu mpya
Kuteuliwa kwa waziri mkuu mpya kunatoa fursa ya kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri, kulingana na katiba.
Rais wa Rwanda amteua waziri mkuu mpya
Justin Nsengiyumva ameeleza uteuzi wake kama heshima kubwa. / Wengine
24 Julai 2025

Rais wa Rwanda Paul Kagame amemteua waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, akimtaja naibu gavana wa benki kuu, Justin Nsengiyumva kuchukua nafasi hiyo.

Uteuzi wa Nsengiyumva, mwenye shahada ya uzamifu ya uchumi, ulitangazwa na msemaji wa serikali katika ujumbe kupitia mtandao wa X siku ya Jumatano.

Ujumbe huo haukusema kwa nini aliyeko sasa madarakani, Edouard Ngirente, ameondolewa. Ngirente, ambaye amekuwa waziri mkuu tangu 2017, alimshkuru Kagame kupitia X, lakini hakueleza sababu za kuondolewa kwake madarakani.

"Safari hii imekuwa yenye tija sana," alisema.

Nchini Rwanda, waziri mkuu ndiye kiongozi wa serikali na ana jukumu la kusimamia shughuli za kila siku za serikali, huku rais akiwa kiongozi wa nchi na mwenye mamlaka kikatiba.

Rwanda ilifanya uchaguzi wake wa mwisho 2024 ambapo Kagame alichaguliwa tena na kura 99.18%.

Waziri Mkuu mpya wa Rwanda ni nani?

Nsengiyumva amekuwa naibu gavana wa Benki Kuu ya Rwanda hadi Jumatano.

Ameahidi kutumikia Rwanda kwa unyenyekevu na bidii.

“Nimepokea jukumu hilo na dhamira yangu ni kuangazia vipaumbele vya nchi yetu. Nitajitolea kwa moyo wangu kukusaidia [rais] katika kutimiza dira ya nchi hii,” Nsengiyumva alisema katika taarifa kwenye X.

Kuteuliwa kwa waziri mkuu mpya kunatoa fursa kwa kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri, kulingana na katiba.

Baraza la mawaziri lazima liteuliwe na rais kwa kushauriana na waziri mkuu katika kipindi cha siku 15.

Nsengiyumva ana shahada ya uzamifu katika uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Leicester. Shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi kuhusu sera ya uchumi na usimamizi na shahada ya biashara kutoka Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki.

Amewahi kuwa katibu mkuu wizara za elimu, biashara na viwanda.

Awali, alifanya kazi katika serikali ya Uingereza kama mshauri mwandamizi wa uchumi, Ofisi ya Reli na Barabara.​​​​​​​

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us