AFRIKA
1 dk kusoma
Wito kwa watendaji wa uchaguzi Tanzania kushirikiana na wadau wote
Tume huru ya uchaguzi Tanzania imewataka watendaji wake kufanya vikao na viongozi wa vyama vya siasa kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa uteuzi wa wagombea unafanyika kwa utaratibu uliowekwa.
Wito kwa watendaji wa uchaguzi Tanzania kushirikiana na wadau wote
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania Jacobs Mwambegele. / Picha:INEC
23 Julai 2025

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania, Jacobs Mwambegele amewataka watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kukutana na iongozi wa vyama vya kisiasa ili kujadili muelekeo wa namna uchaguzi huo utakavyokuwa.

Mwambegele alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya kutoa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi mkoani Shinyanga Jumatano Julai 23, 2025.


“Mtatakiwa kuyatafsiri mafunzo haya kwenye usimamizi wenu wa shughuli za kila siku za masuala ya uchaguzi kwa kuanza na vikao na vyama vya siasa, utoaji wa fomu za uteuzi na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge na kuhakikisha utoaji wa fomu za uteuzi na uteuzi wenyewe ngazi ya udiwani ufanyike kwa mujibu wa sheria,” amesema Mwambegele

Amewaelekeza kuratibu kamati za kampeni na kuitisha kamati za maadili iwapo kuna changamoto zitajitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi.

Mwenyekiti wa tume pia amewataka watendaji kuwa makini wakati wanapotoa taarifa kuhusu mchakato wa uchaguzi.

“Hakikisheni mnajiandaa kabla ya kukutana na vyombo vya habari. Pima taarifa yako unayotaka kuitoa kabla hujaitoa ili kuepuka kuleta taharuki badala ya utulivu katika eneo lako na taifa kwa ujumla,” aliongeza Mwambegele.

Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania imekuwa na mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wake yaliyofanyika katika mikoa mbalimbali nchini humo.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us