Nini Rais Ruto afanye kutatua changamoto za vijana Kenya?
AFRIKA
3 dk kusoma
Nini Rais Ruto afanye kutatua changamoto za vijana Kenya?Maandamano ya Gen Z nchini Kenya yameibua maswali mengi, kubwa ikiwa utendaji kazi wa serikali lakini zaidi ahadi zilizotolewa na uongozi wa Rais William Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi 2022.
Rais William Ruto wa Kenya. / Reuters
23 Julai 2025

Rais wa Kenya William Ruto katika siku za hivi karibuni amejikuta akitetea uongozi wake kutokana na shutma za ukosefu wa ajira kwa vijana, mara nyingi Ruto akisema wanaomuwekea mzigo wa vijana kutokuwa na kazi ni kama ‘jumba bovu’ linatafuta wa kumuangukia.

‘’Watu wanataka kutudanganya kuwa vijana wa Kenya wamekosa ajira ghafla, baada ya mimi kuwa rais. Wote hao walikuwa na kazi kabla ya mimi kuwa rais? Huo siyo ukweli’’ alisema Ruto.

‘’Hatujawahi kuwa na serikali yenye mifumo mizuri na mikakati kama ambayo nimeiweka mimi.Na ndiyo maana tumejaribu kutatua kero za muda mrefu za watu kukosa ajira’’, aliongeza Ruto.

 Rais Ruto anadai maandamano ambayo yamekuwepo hivi karibuni nchini Kenya yana malengo ya kisiasa yakitumia vijana ambao hawana ajira kufikia maslahi yao binafsi.

Anasisitiza kuwa kwa vijana kupata ajira, lazima kuwe na mpango mkakati, na kuwa kazi haziwezi kupatikana kupitia vurugu na uharibifu wa mali au kutatiza amani.

Maandamano ya vijana

Sasa hivi nchini Kenya ukosefu wa ajira unakadiriwa kuwa asilimia 12.7. Miongoni mwa vijana wa kati ya umri wa 15 na 34, ambao wanawakilisha asilimia 35 ya idadi ya raia wa Kenya hali ni mbaya zaidi asilimia 67 kati yao hawana ajira.

Katika maandamano ya hivi karibuni ya vijana baadhi ya madai yalikuwa kushindwa kutimiza kwa ahadi kwa serikali ya Ruto, kubwa ikiwa ukosefu wa ajira kwao.

Mmoja wa walioshiriki katika maandamano ya vijana au maandamano ya Gen Z Roy Shana anasema tatizo lao kwa serikali ni kushindwa kutimiza ahadi.

‘’Serikali badala itupe kazi zile ambazo ilituahidi sisi vijana, kazi wanayofanya ni kutuua kila tunapoandamana kutetea haki yetu’’, alisema Roy Shana.

‘’Sisi wakituambia kazi hizi hapa, njooni mfanye, hautatuona barabarani tena,’’ aliongeza Roy.

Rais Ruto amekuwa akisifia serikali yake akisema wamefanikiwa kupunguza tatizo hilo, kwa mfano kutoa ajira 320,000 kwa vijana katika mradi wa ujenzi wa nyumba nafuu, ajira 400,000 nje ya nchi na 200,000 kwa sekta ya kidijitali.

Mapendekezo ya Raila Odinga

Kiongozi wa chama cha ODM ambaye aliunda serikali ya maridhiano na Ruto, Raila Odinga anasema maandamano hayawezi kuwa suluhu ya matatizo yaliyoko.

‘’Maandamano ya kila siku na kutaka Ruto ajiuzulu hakuwezi kuleta suluhu. Hata Ruto akiondoka leo, haitakuwa suluhu la changamoto zetu. Hata mkimchagua Rigathi Gachagua (aliyekuwa Naibu Rais), hatoleta tofauti yoyote’’, Raila alisema.

Kiongozi huyo anapendekeza kuwepo na majadiliano ya kitaifa, akitaka kuwepo na wawakilishi 40 kutoka kila kaunti katika kaunti zote 47. Wawakilishi hawa wafanye mkutano na Rais Ruto ili kutatua matatizo yaliyopo.

Wanachosubiri kwa sasa ni kama ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi zitatimizwa kiasi cha kuwaridhisha.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us