Ukiona dalili hizi kwa mpenzi wako, jua tayari umeachwa
Ukiona dalili hizi kwa mpenzi wako, jua tayari umeachwa
Mara nyingi vitendo ndivyo vinavyotumika kuliko maneno kuashiria kuwa aliyekuwa mpenzi wako amekuchoka na anataka muachane.
23 Julai 2025

Kwa mujibu wa tafiti, wanandoa au wapenzi, mara nyingi wanakuwa hawajui, ni wakati gani penzi lao linapokuwa limekwisha, au mmoja wao anapokuwa tayari ameachwa bila kupewa taarifa rasmi.

Katika hatua hii, mara nyingi vitendo ndivyo vinavyotumika kuliko maneno.
Hizi ni baadhi ya dalili ambazo, wanasaikolojia wanasema, ukiziona, basi ujue umekalia kuti kavu.

Kukatika au kupungua kwa mawasiliano
Wapenzi mara nyingi wanakuwa na ratiba maalumu ya mawasiliano. Kwa mfano, unakuta pengine, asubuhi ukiamka unaweza kukuta ujumbe unaosema, “Umeamkaje mpenzi? Nakutakia asubuhi njema.”

Mchana pia ujumbe mwengine unaweza kuingia, mara hii wa kukujulia hali na kutaka kujua, siku yako imekuaje.

Kwa hiyo, unapoona utaratibu huu umeanza kubadilika, sio kwa siku moja au mbili, bali umekuwa ni muondelezo, basi jua fika kwamba, mambo yameanza kuharibika.

Katika mazingira haya, utakapojaribu kuhoji, sana sana jibu utakalopewa ni kazi kuongezeka hivyo kushindwa kuwasiliana kama awali.

Ukiona dalili hii, basi kaa chonjo, uje tayari mzigo sio wako.

Hakuangalii usoni
Katika mwili wa binadamu, miongoni mwa viungo visivyoweza kuficha hisia ni macho. Macho mara nyingi yanaenda sambamba na kilichopo moyoni. Kama moyo unasema hapana, basi ni mara chache, macho yatasema ndio.

Unapoona mwenza wake hataki kukuangalia machoni, basi ujue kuna kitu kikubwa anaficha. Kwa sababu sehemu kubwa ya mawasiliano ya wapendanao, ni kuangaliana usoni. Sifa hiyo inapokosekana, basi bila shaka kuna kitu kikubwa kinakosekana.

Hakuweki katika mipango yake ya kila siku
Katika mazungumzo ya kawaida, unaweza kukuta haupo sehemu ya mpango wake wa kila siku.

Anaweza kukuambia, pengine mwishoni mwa juma, ana mpango wa kwenda kufanya manunuzi ya vitu pekee yake, tofauti na ilivyokuwa awali, mlikuwa mnaenda pamoja na mnafanya vitu kadhaa pamoja.

Lakini hivi sasa unakuta amekutoa katika mpango huo.

Hajibu simu au meseji zako kwa wakati
Awali, alikuwa na kawaida ya kujibu aidha simu yako au ujumbe wako kwa wakati. Lakini katika siku za hivi karibuni, umegundua, kila unapotuma ujumbe asubuhi, basi anaweza kuujibu mchana au hata jioni.

Ukimuuliza, anaweza kujitetea kwa kusema, “Kazi zimekuwa nyingi,” au “Pole, nilihisi tayari nimekujibu, kumbe sijautuma ujumbe.

”Katika hatua hii, kwa sababu bado unampenda, unaweza kujipa matumaini kwamba, pengine ni kweli alikuwa na shughuli nyingi. Lakini uhalisia ni kwamba, hizo zote ndio dalili ya mvua.

Ataanza kusahau kumbukumbu muhimu kama siku ya kuzaliwa
Katika mahusiano yoyote, kuna zile tarehe muhimu ambazo siku zote zinawaunganisha pamoja.

Kwa mfano, tarehe mliyoanza mahusiano yenu, siku zote mmekuwa mkiienzi au tarehe yako ya kuzaliwa siku zote imekuwa ni siku ya shamrashamra.

Lakini unapoonza kuona mwenza wako ameanza kuzipa kishogo tarehe hizo, kwa kisingizio cha kusahau, basi ni dalili tosha kwamba, kama zisivyokuwa na umuhimu, basi na wewe pia huna tena huo umuhimu.

Mazungumzo ya kulazimisha
Unakuta mara nyingi mnapozungumza, mazungumzo yenu yanakuwa ni ya kulazimisha.

Mara nyengine, hata mnakosa cha kuongea, kunabaki ukimya.

Hataki kukiri kama kuna tatizo
Katika hali hii, unaweza kujaribu kuanzisha mazungumzo na kumwambia kwamba amebadilika.

Lakini, mara nyingi atakataa katakata kwamba amebadilika, na wakati mwengine hata kuanzisha ugomvi, na kudai kwamba unamsingizia.

Ukikaa kimya…na yeye anaweza kukaa kimya
Siku utakayoamua kumjaribu kwa kukaa kimya bila kumtumia ujumbe, basi utashangaa kuona siku imeisha bila nay eye kukutumia ujumbe.

Unaweza kujiliwaza kwa kusema, pengine mambo yanaweza kubadilika, lakini uhakika ni kwamba, kutokana na dalili hizo uhusiano umekwisha.

Mahusiano yako yamefikia hatua mbaya, ambayo sio rahisi kurekebishika.

CHANZO:TRT Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us