Serikali ya Uganda imesema iko tayari kuwa mwenyeji wa Mashindano ya CHAN 24, yanayoanza mwishoni mwa juma na kufanyika katika nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Serikali ya nchi hiyo imesema kuwa usalama umeimarishwa ipasavyo huku mashabiki wa soka wakitarajiwa kuelekea katika uwanja wa taifa wa Mandela ambao pia unajulikana kama Uwanja wa Namboole, kwa ajili ya michuano hiyo ya (CHAN).
Nchi hiyo imewekeza katika kuimarisha uwanja wake wa taifa wa Namboole uliopo katika wilaya ya Wakiso, kilomita kadhaa kutoka jiji la Kampala.
Katika miezi ya hivi karibuni, Uwanja wa Taifa wa Mandela, Namboole uliofunguliwa 1997, umepitia marekebisho makubwa kama sehemu ya maandalizi ya CHAN.
Iwapo uwanja huo utajaa, basi mashambiki 38,000 wanatarajiwa kushuhudia mechi ya kwanza ya CHAN itakayochezwa Agosti 4 kati ya Uganda na Algeria.