Robert Francis Prevost amechaguliwa kuwa Papa wa kwanza kutoka Marekani, Vatican imetangaza.
Anaaminika kuwa na msimamo wa kadri na alikuwa mshirika wa karibu wa Papa Francis na kwa miaka mingi alihudumia Kanisa nchini Peru, anakuwa Kiongozi wa 267 wa Kanisa Katoliki, akichukuwa jina la Kipapa la Leo XIV.
Makadinali walimchagua Papa mpya kuongoza Wakatoliki bilioni 1.4 duniani siku ya Alhamisi, na moshi mweupe kuonekana kutoka Kanisa la Sistine katika siku yao ya pili ya upigaji kura.
Maelfu ya watu waliokuwa katika medani ya Mtakatifu Peter walisherehekea,na wengine wakilia kwa furaha wakati moshi huo ulipoonekana, na mlio wa kengele kusikika.
Makundi ya watu yalikimbilia sehemu ya medani kutizama juu kwenye roshani ambayo ilikuwa imepambwa kwa pazia nyekundu kwa ajili ya hotuba ya kwanza kwa dunia ya Papa wa 267.
Mrithi wa Papa Francis
Papa huyo mpya, ambaye anamrithi raia wa Argentina aliyeleta mabadiliko Papa Francis, alitambulishwa kwa lugha ya Kilatini na jina ambalo amechaguwa na kuhutubia dunia kwa mara ya kwanza.
"Ni jambo la kufurahisha," alisema Joseph Brian akieleza furaha yake, mpishi mwenye umri wa miaka 39 kutoka Belfast huko Ireland ya Kaskazini, ambaye amekwenda jijini Rome pamoja na mama yake kushuhudia tukio hilo.
"Mimi si mtu wa dini sana, lakini kuwepo hapa na watu wote hawa, kumenipa faraja sana," ameiambia AFP huku watu waliokuwa karibu na yeye wakirukaruka kwa furaha.
Kulikuwa na hali ya furaha kwa watu wengi huku padre mmoja akikaa juu ya mabega ya mtu na kupeperusha bendera ya Brazil, na mwingine akionesha alama ya Yesu akiwa msalabani kama ishara ya furaha yake.