Nchini Ethiopia kuna jamii yenye utamaduni wa kipekee. Kusini-magharibi mwa Ethiopia, kabila linaloitwa Banna hutembea kwa miti.Naam!Hapa kutembea kwa miti namna hii ni kawaida sana hasa kwa vijana.Vijana, wanaojulikana kama "Tewa," awali walitumia miti hii ili kujilinda dhidi ya nyoka na wanyama wengine hasa wanapochunga ng’ombe wakiwa porini.
Hii pia ilitumika kama mbinu ya usalama pindi wanapotembea kwenye udongo uliolowa au kwenye vichaka.
Baada ya muda, mazoezi haya yakawa sehemu muhimu ya utambulisho wao wa kitamaduni, haswa wakati wa sherehe tofauti.
Kutembea kwa miti mirefu ikawa ndio utambulisho wa kitamaduni ukiashiria vijana kutoka katika rika moja hadi jengine.
Tewa hutengeneza miti yao kutoka miti ya asili, kamba, na mikanda ya ngozi.
Kwa urefu inaweza kuwa hadi mita mbili.
Vijana hujifunza kutembelea miti kwa miaka mingi tangu wakiwa wachanga.
Maonyesho yao pia yamekuwa ni kivutio kikubwa na chanzo kikuu ya mapato, hivyo kuwa sehemu ya kukuza uchumi wa ndani na nje.
Kama uthibitisho wa kuwa tayari kuingia katika rika la utu uzima, basi vijana sharti waonyeshe umahiri wao katika sherehe ya kuruka ng’ombe kwa kutumia miti hiyo.
Ili kuonyesha utayari wa kuchukua madaraka ya utu uzima,kijana kutoka kabila la Banna anaweza kulazimika kuruka hadi ng’ombe 15 kwa mara moja.
Ili kufanikiwa katika hilo, vijana kila siku wanafanya mazoezi ya kujenga mwili.Wakati wa harusi, pia hutumika kuburudisha wageni na kuongeza shamra shamra.
Maonyesho haya pia husaidia kuweka mila zao hai na kuunganisha jamii.
Baadhi wanaamini kwamba, watembea kwa miti ni kiunganishi kati ya dunia na mbingu.
Zaidi ya yote, utamaduni huu unakuza fahari ya kipekee kati ya watu wa kabila la Banna na kila wakati kuwakumbusha urithi wao.