Hii ni mara ya kwanza kwa michuano hii kuwa na nchi mwenyeji zaidi ya moja, ikiwa ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Mechi ya ufunguzi itakuwa siku ya Jumamosi ambapo Taifa stars ya Tanzania itakabiliana na Burkina Faso.
Mashindano haya ya CHAN ni ya nane na yamekuwa yakiimarika mara kwa mara huku viwango vikionekana kuwa vya juu miongoni mwa wachezaji.
Wenyeji mwenza Kenya wataanza kampeni yao dhidi ya mabingwa mara mbili wa michuano hiyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Jumapili.
Jumatatu itakuwa zamu ya Uganda kukipiga dhidi ya Algeria kwenye kundi C.
Mbali ya zawadi ya fedha inayotolewa na shirikisho la soka barani Afrika CAF ambapo mshindi ataondoka na kitita cha dola milioni 3.5 baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania zimeahidiwa zawadi kede kede.
Nafasi ya pili ataondoka na dola milioni 1.2 huku nafasi ya tatu akibeba dola laki saba.
Miongoni mwa mataifa yote kumi na tisa kila timu ina matumaini kuwa itaondoka na ushindi wakati fainali hizo zitakapochezwa jijini Nairobi.
Kwa sasa macho yote yako Tanzania siku ya Jumamosi kwa ajili ya mechi ya ufunguzi.