Mataifa yanayoendelea yanakabiliana na changamoto kubwa za ufadhili.
Tatizo la sasa limetokana na Marekani kusitisha misaada kwa ghafla, na inaonesha mtindo wa kupunguzwa kwa ufadhili katika miaka ya hivi karibuni.
Ni wakati wa kutafakari kuhusu mifumo ya misaada — hasa kwa kuwa inajenga tabia ya utegemezi zaidi.
Nchi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitegemea misaada kutoka nje sasa zinabidi kutafakari kuhusu sera zake.
Kwa mataifa yenye matatizo makubwa kwa raia wake, kupunguzwa kwa misaada hii kutakuwa na athari mbaya zaidi.
Kwa hili, kuwepo kwa umoja wa jamii ya kimataifa na kusaidiana kifedha ni muhimu sana.
Lakini kwa wengine, kipindi hiki kinatoa fursa ya kuangalia upya fursa zingine za kujiendeleza.
Eritrea ni nchi ambayo mara nyingi inaonekana kama imetengwa, kuna mambo kadhaa mataifa mengine yanaweza kujifunza kutoka kwa nchi hiyo kuhusu kujitegemea na kufanya maendeleo kwa kutumia raslimali chache.
Kulingana na ushirikiano wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo, hapa kuna mambo matano ya kujifunza kutoka kwa mfumo wa Eritrea ambao huenda ukawa muhimu wakati huu:
1. Weka malengo yako mwenyewe ya maendeleo
Eritrea imekuwa imara katika kuhakikisha kuwa misaada kutoka nje inalingana na vipaumbele vyake kama taifa, msimamo uliowafanya wawe na udhibiti makini wa mipango yake ya maendeleo kuliko kutegemea maelekezo ya wafadhili yanayobadilika mara kwa mara.
Ni muhimu kutambua kuwa kujitegemea hakumaanishi kujitenga. Eritrea ina washirika mbalimbali — ikiwemo Italia, China, Uingereza, na Japan. Umoja wa Mataifa umekuwepo katika nchi hiyo kwa muda mrefu na leo hii unafadhili miradi ya nishati ya jua, elimu, afya, upatikanaji wa chakula cha kutosha, masuala ya tabianchi, na zaidi. Ushirikiano huu unafanyika kutokana na vipaumbele vya maendeleo ambavyo Eritrea yenyewe imejiwekea pamoja na uongozi wake.
2. Mitazamo ndani ya nchi: Imarisha raslimali za nyumbani
Wakati Eritrea ilipositisha shughuli za shirika la USAID 2005 (Financial Times), wengi walihoji kama nchi hiyo itaweza kujiendeleza bila misaada kutoka nje. Karibu miongo miwili baadaye, Eritrea imetegemea raslimali zilizoko ndani ya nchi, ikisisitiza matumizi ya msingi, ustawi wa jamii, na mtazamo endelevu. Mapato ya kodi, fedha zinazoletwa na raia kutoka nje ya nchi, uwekezaji wa mashirika ya umma katika kilimo, afya, na nishati endelevu ni masuala ambayo yamechangia pakubwa mfumo wake.
3. Kuzingatia maslahi ya watu kwanza
Eritrea imeangazia maslahi ya watu kwa kuwapa huduma za msingi na ustawi wa jamii, na kupiga hatua katika elimu, huduma ya afya, na upatikanaji wa chakula cha kutosha. Ilikuwa ni moja kati ya nchi chache zilizofanikiwa kutimiza malengo yake ya milenia (MDG) katika suala la afya.
Mfano wa ubunifu wao ni njia ambayo wanavyofikia jamii zilizo vijijini kabisa kwa kuwapeleka wahudumu wa afya ambao wamepewa mafunzo kuwapa matibabu wanavijiji —hatua iliyosaidia pakubwa kuimarisha afya za watu ambao kufikiwa si rahisi. Zaidi ya hayo, hatua ya Eritrea kuweka msisitizo kwenye masuala ya haki za wanawake na usawa —kutokana na historia yao wakati wa mapambano ya uhuru — inadhihirika kwenye sera zao ambazo zinaendeleza upatikanaji wa fursa za elimu na kiuchumi kwa wanawake na wasichana.
Kuhamasishwa kwa kampeni za chanjo kumesaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa, huku juhudi za kuhifadhi maji na udongo zimesaidia upatikanaji wa chakula cha kutosha. Hatua hizo zinaonesha namna gani ukielenga kuwekeza zaidi kwa watu kunaweza kuleta matokeo ya kudumu kwa maendeleo.
4. Shirikisha raia katika suala la maendeleo
Eritrea ina idadi ndogo ya watu lakini wamehamasishwa kupitia utamaduni thabiti wa majukumu ya raia na ushirikishwaji. Kwa mfano, ujenzi wa mabwawa madogo kwa ajili ya kuhifadhi maji na kilimo unaongozwa na jumuiya zenyewe. Mtazamo huu unajenga hali ya umiliki na mfumo endelevu wakati pia wakihakikisha gharama za chini na kupunguza ubadhirifu.
Viwango vya ufisadi ni vya chini sana (The Guardian), hii inamaanisha kila fedha inayowekezwa na washirika wa maendeleo inafikishwa sehemu husika kama inavyotakiwa.
5. Mipango ya muda mrefu na kuwa na ustahmilivu
Eritrea imeyapa kipaumbele masuala ya uendelevu na ustahmilivu. Uwekezaji katika nishati ya jua, ujenzi wa mabwawa, na kuhifadhi udongo kumefanya wapunguze kutegemea bidhaa kutoka nje na misaada ya kigeni. Umoja wa Mataifa umeunga mkono juhudi hizi, hasa katika miradi ya tabianchi ambayo inasaidia kuimarisha kilimo.
Huku uhaba wa fedha ukitatiza juhudi za maendeleo kote duniani, uthabiti - katika masuala ya tabianchi, kilimo endelevu, na upatikanaji wa nishati — yanakuwa masuala muhimu zaidi.
Hatimae
Mtazamo wa ufadhili ulimwenguni umebadilika, na serikali nyingi zinapitia changamoto za kutafuta mbinu za kukabiliana na kupungua kwa fedha kutoka mataifa ya kigeni. Eritrea ina mawazo mbadala kwa suala la maendeleo, na kulitilia msisitizo jambo hilo ni mchakato muhimu zaidi.
Pamoja na kuwa misaada kutoka nje yanaweza kuchangia pakubwa mabadiliko, maendeleo endelevu yanasimamiwa vizuri na jamii na mifumo ya kitaifa yanaotoa dira ya njia zao wenyewe.
Mfumo wa Eritrea pia siyo rahisi. Namna walivyoweka udhibiti katika masuala ya siasa na uchumi unawafanya wanakuwa tofauti na mataifa mengine.
Sekta binafsi haijakuwa sana, ambapo ni kikwazo kwa ubunifu, ukuaji wa uchumi, na upatikanaji wa ajira —hasa kutokana na kuwa idadi ya watu inaongezeka. Masuala mengine kama vile kuimarisha kuwepo na sera mahsusi, huenda kukasaidia kufungua njia za uwekezaji wa kigeni.
Na huku Eritrea ikiangalia mbele, kwa kuwa na msingi imara wa uchumi, itakuwa muhimu kwa mafanikio ya maendeleo kutoa taswira ya maisha bora kwa watu na fursa za kiuchumi kwa kila mtu.
Hata hivyo, katika dunia ambayo uhaba wa fedha unaonekana ndiyo hali ya kawaida, falsafa ya Eritrea ya kujitegemea ni funzo muhimu kuhusu namna serikali zinaweza kushughulikia maendeleo yao kwa ufadhili mdogo kutoka mataifa ya nje.
Na huku nchi duniani zikitathmini kuhusu misaada ya washirika wa maendeleo, mifumo ya Eritrea yanatoa mafunzo ambayo ni muhimu kuzingatiwa.
Mwandishi, Nahla Valji ni Mratibu wa Misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Eritrea
Kanusho: Maoni ya mwandishi hayaakisi maoni, mitazamo na sera ya uhariri ya TRT Afrika.