Januari 2025 waasi wa M23 walifanya mashambulizi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC na kudhibiti maeneo kadhaa. Baadhi ya maafisa wa jeshi la serikali na polisi wa serikali ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walikimbilia kituo cha Umoja wa Mataifa kilichopo Goma.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) unasema sasa umeanza operesheni ya kuwasafirisha mamia ya wanajeshi wasio na silaha wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC), Polisi wa Kitaifa wa Congo (PNC), na baadhi ya watu wanaotegemewa waliokimbilia vituo vyao huko Goma.
Maafisa hao wanapelekwa hadi Kinshasa.
“Operesheni hii inafuatia zaidi ya miezi mitatu ya ulinzi endelevu unaotolewa na MONUSCO kwa maafisa wa FARDC na PNC ambao walikuwa wamekimbilia katika vituo vyake tangu M23 ilipochukua udhibiti wa Goma mwishoni mwa Januari 2025, ” Bruno Lemarquis, Naibu Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa DRC na Kaimu Mkuu wa MONUSCO amesema.
Operesheni hii inafanywa kwa usaidizi wa vifaa wa MONUSCO na inawezeshwa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) katika jukumu lake kuu kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote.
Kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa, watu wote chini ya ulinzi wa MONUSCO walikuwa wamepokonywa silaha.
UN imesema oparesheni hiyo itafanyika kwa siku kadhaa na itajumuisha misafara mingi.
Usafirishaji wa wanachama wa FARDC na PNC unafanywa hadi Kinshasa, ambapo wataungwa mkono na mamlaka ya kitaifa, unafanywa kwa idhini yao na chini ya ulinzi wa Mikataba ya Geneva.
Lemarquis anatoa wito kwa pande zote husika kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha mafanikio ya operesheni hii tata.