Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesisitiza kuwa Gaza ni mali ya Wapalestina, kama ilivyo kwa eneo la Ukingo wa Magharibi na Yerusalemu.
"Kama ilivyo tu kwa Yerusalemu Mashariki na Ukongo wa Magharibi, Gaza ni mali ya Wapalestina. Mungu akipenda, ndugu zetu wa Gaza wataendelea kuishi kwenye ardhi waliyozaliwa," alisema Erdogan baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Ankara siku ya Jumatatu.
Akikosoa udhalimu wa Israeli huko Gaza, Erdogan alisisitiza kuwa hakuna kitakachofikiwa iwapo umwagaji damu na vitendo vya kusitisha misaada ya afya na chakula vitaendelea.
"Ni lazima ifahamike kuwa hakuna hatua itakayofikiwa iwapo kwa kuendelea kumwaga damu huko Gaza, mauaji ya zaidi ya watoto, na watu kushinda njaa bila madawa," alisema.
Udhalimu wa Israeli
Tangu Machi 2, Israeli imezuia misaada ya vyakula, madawa na misaada mingine ya kibinadamu kuingia Gaza na kufanya hali ya kibinadamu iwe mbaya zaidi.
Zaidi ya Wapalestina 52,200 wameuwawa huko Gaza, wengi wakiwa ni wanawake na watoto, toka kutokea kwa machafuko ya Oktoba 2023.
Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa kibali cha kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu pamoja na Waziri wake zamani wa ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Gaza.