Kocha wa Inter Milan simone Inzaghi amemsifia mchezaji wa Barcelona Lamine Yamal baada ya mchezo mzuri wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kumalizika kwa sare ya 3-3 siku ya Jumatano.
Yamal, 17, alifunga goli moja katika mechi yake ya 100 na Barcelona wakati timu hiyo ikikomboa na mara nyingi akiwapa tabu wachezaji wa safu ya ulinzi wa Inter.
"Bila shaka Yamal ni mchezaji hodari sana, ni yule mchezaji anayezaliwa baada ya kila miaka 50 tu, uhodari wa aina hii sijawahi kuuona," alisema Inzaghi.
"Nimemuona leo kwa mara ya kwanza na ametupa tabu sana, tumemuwekea wachezaji wawili kumkaba... alafu tukashindwa kuweka wachezaji wengine sehemu zingine za uwanja...
‘Kujipongeza’
"(Namna tulivyocheza) ni jambo la kujipongeza, na Yamal ni mchezaji wa kipekee ambao mahodari aina hii wanazaliwa baada ya kila miaka 50 tu."
Inter walijitahidi kumbana Yamal kwa sehemu kubwa ya kipindi cha pili, ambapo Inzaghi anasema ndilo lilokuwa lengo baada ya mchezo wake wa kipindi cha kwanza.
"Tulifanya marekebisho kidogo, ilibidi tutafute mbinu ya kumdhibiti Yamal, na haikuwa rahisi," aliendelea kocha huyo.
Inzaghi pia alisema kuwa "kuna wasiwasi" kama nahodha Lautaro Martinez, ambaye alitolewa kutokana na majeraha, kama hali yake itakuwa imeimarika kwa hatua ya fainali ya pili.
Kulinganishwa na Messi
Kocha wa Barcelona Hansi Flick alimsifia winga huyo Yamal, aliyekataa kulinganishwa na mchezaji bora Lionel Messi siku moja kabla ya mechi, lakini akafunga goli ambalo Muargentina huyo angelilifurahia sana.
"Nimefurahi sana kuwa uhodari huu ambao unatokea baada ya kila miaka 50 kwa Barca," alisema Flick, alipoelezwa kuhusu aliyoyasema Inzaghi.
Kocha huyo Mjerumani alisema Yamal alihamasisha timu yake kusawazisha.
"Katika kipindi cha kwanza Lamine alikuwa muhimu sana kwetu, alikuwa na ubunifu sana na kufunga goli la kwanza," Kocha huyo Mjerumani aliwaambia waandishi wa habari.
"Katika mechi kubwa unaona uhodari wa mchezaji huyu na ameuonesha hii leo, ni mchezaji mzuri kuwa naye kwenye timu.. .
"Ni hodari sana,... unaona kila anachokifanya na inashangaza namna anavyofanya."