Kwa nini ukosefu wa ajira bado ni 'pasua kichwa' kwa serikali ya Kenya
MAISHA
6 dk kusoma
Kwa nini ukosefu wa ajira bado ni 'pasua kichwa' kwa serikali ya KenyaVijana sita kati ya kumi nchini Kenya wamekosa ajira, jambo linalowapelekea kupaza sauti zao dhidi ya uongozi wa Rais William Ruto, kama inavyojidhihirisha kupitia maandamano na machapisho mitandaoni.
Vijana Kenya walipinga ufisadi 17 Februari 2006/ Picha: Reuters
28 Julai 2025

Juni 25, 2024, Kenya na ulimwengu mzima ulishuhudia maandamano makubwa dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Maandamani hayo yaliongozwa na kuratibiwa na vijana, ambao kwa uwingi wao, waliingia mitaani, kushinikiza kubatilishwa kwa Muswada wa Fedha wa mwaka 2024.

Shinikizo hilo lilifanikiwa, na hatua hiyo ikazaa maandamano mengine ya vijana, ambao wana tamaa ya kuona mabadiliko ndani ya taifa hilo.

"Tusidanganyike kuwa vijana tunaowaona mitaani wakidai mabadiliko kutoka kwa serikali wote si wasomi, hapana, wengi wamesoma sana, hawana tu nafasi za ajira" aelezea Caroline Njeri, mjasiriamali katika Kaunti ya Nakuru.

Binti yake Delia ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Egerton katika Kaunti ya Nakuru akifanya masomo ya Kilimo.

"Licha ya binti yangu kuwa na astashahada, nilimuhimiza achukue shahada ili awe katika nafasi nzuri ya kujipatia ajira kwani kuna ushindani mkubwa sana nchini Kenya,” anaeleza Njeri katika mahojiano na TRT Afrika.

Kwa sasa, Delia ana umri wa miaka 28, ambao ni wastani wa umri wa vijana wa ‘Gen Z’, ambao wamekuwa wakiiandama serikali tangu mwaka 2024.

"Unakweda kuomba kazi unaambiwa hakuna , nimejaribu kuanzisha biashara zetu mwenyewe lakini mahitaji ya mtaji ni makubwa sana, hivyo baadhi yetu tunaamua kurejea shule," Delia anasema.

Delia anasema kuwa anaona vijana wengi wakipoteza matumaini ya kusoma kwa sababu wanaona hakuna fursa za ajira.

Ajira ilikuwa ni moja ya ahadi kuu za William Ruto, wakati akisaka nafasi ya kuiongoza nchi hiyo.

"Tuna vijana milioni 4 ambao wamemaliza elimu na ikiwa hatutatengeneza ajira wanaweza kuwa ‘bomu’ kwa nchi yetu," alisema Ruto, miaka mitatu iliyopita.

"Mwaka ujao (2023) tutawekeza shilingi bilioni 100 katika miradi na mipango ambayo itawapa vijana wetu ajira milioni 4."

Kwa wakati huo, kauli mbiu yake ilikuwa ni ‘vuguvugu la hustler’, lililokuwa limelenga kuwainua watu wa kada mbalimbali, waliokuwa wanataabika na maisha.

Miaka miwili baadaye, jinamizi la ukosefu wa ajira kwa vijana, bado linamghubika Rais William Ruto.

Kwa nini ukosefu wa ajira unaendelea?

Ukosefu wa ajira nchini Kenya haukuanza kipindi cha utawala wa Rais Ruto, bali ni changamoto iliyokita mizizi kwenye tawala zilizopita.

Kulingana na Shirikisho la Waajiri wa Kenya "licha ya kuwa ukosefu wa ajira kwa jumla nchini Kenya ni asilimia 12.7, vijana kati ya umri wa miaka 15 na 34, ambao hujumuisha asilimia 35 ya idadi ya watu nchini Kenya, bado wana kiwango cha juu zaidi cha ukosefu wa ajira cha asilimia 67.

Hii ina maana kwamba kwa kila vijana kumi 6 hawana kazi.

Wataalamu wa masuala ya ajira wanasema zaidi ya vijana milioni moja huingia katika soko la ajira kila mwaka bila ujuzi wowote baadhi yao wakiwa wameacha shule bila kujiunga na chuo chochote.

"Ninakubali kwamba tuna changamoto ya ukosefu wa ajira nchini Kenya na inabidi tuwe na nia ya kujua ni wapi tunatengeneza nafasi za kazi. Mojawapo ni nafasi ya usindikaji wa bidhaa za kilimo," alisema Rais Ruto mwezi Juni 2025.

"Moja ya sababu kuu ni ukosefu wa fursa za kutosha au sawa, kazi nyingi za watu weupe tayari zimeshikwa na watu ambao pia ni vijana na kuna fursa ndogo zilizoundwa," anasema Camila Wangoi, Meneja Masoko ambaye hufanya kazi na vijana.

Kulingana na Wangoi, nafasi za ajira bado ni chache sana.

"Kupitia teknolojia ya mitandao ya kijamii, wengi wamejitokeza kujaribu kutengeneza chanzo cha mapato kupitia majukwaa ya mitandao. Hata hivyo, bado haitoshelezi kwani kwani biashara za mitandaoni ziinawapendelea wale wa maeneo ya mijini ambapo vijana wanaweza kupata taarifa kwa urahisi,” anaongezea.

Wangoi anasema kuwa baadhi ya makampuni bado yanajishughulisha na shughuli za kawaida ambazo haziwezi kutengeneza nafasi zaidi za kupitia uvumbuzi wa kidijitali.

Hali kadhalika, wapo baadhi ya Wakenya ambao wanalaumu ushuru mkubwa wa waajiri.

"Kwa mfano kampuni ya kigeni inalipa kama asilimia 37 ya kodi ya shirika, kampuni ya Kikenya mkazi ina zuio la asilimia 30 ya ushuru wa kampuni, ambayo ni gharama moja tu kwa kampuni moja. Kabla hata hawajafikiria kuongeza uzalishaji wao wa kazi mapato yao yamepunguzwa sana na ushuru," anasema Patrick Babu, Mshauri wa masuala ya Mawasiliano.

"Kijana ambaye anataka kuanzisha kazi kwa mfano hivi sasa atakuwa na wakati mgumu chini ya mfumo wa sasa wa kodi katika nchi yetu," anasema Babu.

Kwa upande wake, Immaculate Wacera, mtaalam wa masuala ya fedha anasema serikali ya Kenya imeshindwa kuwalinda raia wake dhidi ya gharama kubwa za maisha.

"Hakuna mazingira mazuri kwa waliojiajiri kufanya biashara kwa sababu ya kodi kubwa, gharama kubwa ya kufanya biashara,” anasema.

Mwezi Aprili mwaka huu, msajili wa kampuni alitangaza kwamba serikali ilikuwa imefuta kampuni 62, na kuzionya zingine 133, kwa kushindwa kutimiza matakwa tarajiwa.

Hatua hii ilipelekea baadhi ya watu kupoteza ajira zao, hasa katika huduma za fedha, mali isiyohamishika, ujenzi na uwekezaji wa ardhi, na wengine walikuwa wanafanya biashara ya kilimo.

"Mashirika mengi na makampuni yamelazimika kufunga biashara na shughuli zao nchini Kenya kutokana na gharama za uendeshaji kuwa juu,” anaongeza Wacera.

Kwa upande wake, serikali ya Rais William Ruto inasisitiza kuwa bado ina mpango wa kukabiliana na ukosefu wa ajira.

Kulingana na Ruto, huo ni mchakato unaokwenda hatua kwa hatua.

Ruto mwenyewe anasema kuwa, zaidi ya vijana 400,000 wamepata ajira nje ya nchi huku serikali ikidai kuwa na mazungumzo na Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani na Ujerumani katika kutengeneza fursa hizo za ajira.

Kiongozi huyo, amesisitiza mpango wake wa kutengeneza nafasi za ajira kwenye miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa serikali yake ambao unalenga kujenga nyumba za bei nafuu kote nchini.

Kulingana na Ruto, vijana wapatao 320,000 wamepata ajira kupitia mchakato huo, huku akisema kuwa serikali yake imenuia kuongeza idadi ya wafanyakazi wa makazi.

Ameongeza kuwa, vijana wengine 180,000, wanapata mapato kupitia maabara za kidijitali zilizoanzishwa na serikali.

Serikali inasema imeajiri walimu 76,000 na ina mpango wa kuajiri 24,000 zaidi, ifikapo Januari 2026.

Wananchi wanapendekeza nini?

"Njia bora ya serikali kukabiliana na ukosefu huu wa ajira kwa vijana ni kupunguza kodi hatua kwa hatua na pia kutoa nafuu ya kodi kwa makampuni makubwa na pia makampuni madogo na ya kati. Hatua hiyo itaweza kupanua biashara na kujitengenezea mapato,” Wacera anaeleza.

Anasema kutafuta vibarua ya nchi si mbaya lakinmi inafaidi wachache tu, hivyo ingekuwa vyema kama ujuzi huo ungehimizwa kusalia nchini.

"Kama kiwanchoi cha ushuru kitarekebishwa, ikiwa serikali itawaepusha wananchi dhidi ya kupanda kwa gharama ya maisha duniani basi tutasonga mbele kwa kasi sana. Kenya ni kiongozi wa kiuchumi katika eneo hili na katika Afrika mambo mengi, lakini ni ukosefu wa mazingira hayo wezeshi ambayo yanawawekea vikwazo kwa vijana hawa wanaofanya kazi kwa bidii," Wacera anaongeza.

Vijana wengine wanapendekeza kwamba makampuni yajitahidi kufanya shughuli zao kwa kisasa na ufanisi zaidi, ili waweze kuajiri vijana wengi kusimamia uzalishaji wao kwa ushindani.

Anapoumiza kichwa ili binti yake amalizie miaka mitatu ya chuo, sala kubwa ya Caroline kwa sasa ni kuona ile dhana ya ‘namjua fulani ili nipate ajira’ inatokomezwa.

Kulingana na Caroline, mashirika ya umma yanapaswa kupunguzia wafanyakazi umri wa kustaafu ili kuwapa nafasi vijana, na pia kuwe na njia ya vijana kutiwa moyo.

Anapendekeza uanzishwaji wa miradi tofauti katika kila kaunti ya kuwapa vijana nafasi ya kujiajiri kutumia ujuzi na ubunifu wao.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us