Watu wasiopungua 21 waliuawa Jumapili katika shambulio lililofanyika kwenye eneo la kanisa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulingana na kiongozi wa jamii ya kiraia.
Shambulio hilo lilitekelezwa na wanachama wa kundi la waasi la Allied Democratic Force (ADF) majira ya saa saba usiku ndani ya eneo la kanisa Katoliki mashariki mwa Komanda, DR Congo. Nyumba kadhaa na maduka pia yalichomwa moto.
"Zaidi ya watu 21 walipigwa risasi na kuuawa ndani na nje ya kanisa, na tumerekodi miili mitatu iliyoungua vibaya pamoja na nyumba kadhaa zilizochomwa moto. Hata hivyo, juhudi za utafutaji bado zinaendelea," alisema Dieudonne Duranthabo, mratibu wa jamii ya kiraia huko Komanda, alipoongea na Shirika la Habari la Associated Press.
Msemaji wa jeshi la Kongo katika jimbo la Ituri, ambako Komanda iko, alithibitisha vifo vya watu 10.