Polisi wanasema wote waliofariki na baadhi ya wale waliojeruhiwa walisafirishwa hadi mji mkuu wa Kenya, Nairobi kwa ajili ya kuhifadhiwa na hatua zingine kuchukuliwa.
Wafanyakazi hao wote watano wa timboni waliuawa siku ya Jumanne asubuhi,wakiwa njiani kuelekea kazini katika kijini kimoja, Kaunti ya Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Polisi wanasema waliouawa walikuwa wameondoka katika mji waliokuwa bila kufahamisha maafisa wa usalama, kama ilivyo kawaida ya eneo hilo. Wote walikuwa ndani ya usafiri wa umma.
Dereva na kondakta wa gari hilo la usafiri wanahojiwa na polisi
Polisi katika eneo hilo wanahusisha tukio hilo la mashambulizi ya wapiganaji wa al-Shabaab ambao inasemekana walionekana kwenye eneo hilo.
Wote waliouawa ni wenyeji wa mikoa mingine ambao walikuwa wanafanya kazi kwenye kwenye matimbo.
Polisi waliofika kwenye eneo la tukio wanasema walipata maganda 39 ya risasi.
Hii si mara ya kwanza kwa tukio kutokea kwenye eneo hilo licha ya kufanyika kwa operesheni ya kukabili vitisho vya al-Shabaab.
Walioshuhudia wanasema washambuliaji walikuwa na bunduki na kuwaamuru wafanyakazi wote kulala chini.
Kisha wakawafyatulia risasi kwa karibu.
Taarifa kutoka makao makuu ya polisi inasema maafisa zaidi wamepelekwa katika eneo hilo kufuatilia kuhusu tukio hilo.
Mauaji hayo yamesababisha wasiwasi na hofu miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho, huku mamlaka zikifika kwenye eneo la tukio kuanza uchunguzi.