ULIMWENGU
2 DK KUSOMA
Mashambulizi ya anga Nigeria yawaua 'makamanda wakuu' wa kundi la kigaidi
Takriban wanamgambo 30 waliuawa wakiwemo makamanda wakuu wa kundi hilo Ali Dawud, Bakura Fallujah na Mallam Ari, jeshi lilisema.
Mashambulizi ya anga Nigeria yawaua 'makamanda wakuu' wa kundi la kigaidi
Jeshi la Nigeria limekuwa likishambulia wanamgambo wa ISWAP mara kwa mara. Picha: Reuters / Others
17 Aprili 2024

Vikosi vya usalama vya Nigeria vimewaua makumi ya wanamgambo wakiwemo makamanda kadhaa wakuu wa kundi la kigaidi la ISWAP kaskazini mwa nchi hiyo, jeshi lilisema Jumanne.

Jeshi la Wanahewa la Nigeria lilifanya mashambulizi ya anga katika jimbo la Kaskazini-mashariki la Borno yakilenga maficho ya kundi hilo kwenye mwambao wa ziwa Chad, taarifa ya jeshi ilisema.

ISWAP ni kundi lililojitenga na Boko Haram. Wamekuwa wakiendesha uasi nchini Nigeria na nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad na kuua maelfu ya raia na vikosi vya usalama na pia kuwafukuza mamilioni ya wengine.

"Operesheni hiyo imedunisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa kundi la ISWAP katika kanda," Jeshi la Wanahewa la Nigeria lilisema katika taarifa.

Wanamgambo wauawa

Mashambulizi hayo ya anga katika kijiji cha Kolleram yalitekelezwa siku ya Jumamosi lakini yakatangazwa kwa umma Jumanne.

Takriban wanamgambo 30 waliuawa wakiwemo makamanda wakuu wa kundi hilo Ali Dawud, Bakura Fallujah na Mallam Ari, jeshi lilisema.

"Mashambulizi haya ya anga yanawakilisha hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Nigeria," ilisema taarifa hiyo.

Shambulio hilo la bomu liliharibu kituo muhimu kinachotumiwa na kikundi hicho kwa shughuli za usindikaji wa chakula, iliongeza.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us