Nchi za Afrika zinavyojiandaa na ‘adhabu ya ushuru’ kutoka serikali ya Donald Trump
SIASA
3 dk kusoma
Nchi za Afrika zinavyojiandaa na ‘adhabu ya ushuru’ kutoka serikali ya Donald TrumpKwa sasa, nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na hali ya sintofahamu kufuatia uamuzi wa serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza hatua ya kuziwekea viwango mbalimbali vya ushuru.
Kulingana na wachambuzi, mkakati huu unalenga kujenga ustahimilivu wa kiuchumi wa bara la Afrika./Picha: Wengine / Others
9 Aprili 2025

Rais wa Marekani, Donald Trump amesisitiza kuwa hatobadili maamuzi yake ya kutengua viwango vya ushuru alivyovitangaza hivi karibuni, huku kukiwa na hofu kubwa ya kuporomoka kwa masoko na biashara kimataifa.

Kwa sasa, mataifa mengi ulimwenguni yameduwazwa na maamuzi haya ya Rais Trump.

Hata hivyo, nchi za Afrika ndio zipo kwenye changamoto kubwa ya kukubaliana na mabadiliko haya mapya na ya ghafla.

Marekani inasema kuwa zaidi ya nchi 50 zimepeleka ombi la kufanya mazungumzo na serikali ya Trump, hali yenye kuashiria hofu kubwa inayotokana na maamuzi hayo.

Hatua ya Zimbabwe

Kwa upande wake, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amechukua maamuzi ya kusitisha ushuru kwenye bidhaa zitokazo Marekani kwa nia ya kukuza bidhaa hizo na zile za Zimbabwe zenye kuuzwa nchini Marekani. Kulingana na sera hiyo ya Trump, Zimbabwe inakabiliwa na ongezeko la asilimia 18 ya ushuru.

“Uamuzi huu unalenga kuwezesha uuzwaji wa bidhaa za Marekani ndani ya soko la Zimbabwe na vile vile kukuza bidhaa za Zimbabwe,” alisema Rais Mnangagwa kupitia ukurasa wake wa X.

Wajumbe wa Lesotho wakimbilia Marekani

Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Lesotho.

Huku asilimia 45 ya bidhaa zake za nguo ikienda Marekani, nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na asilimia 50 ya ushuru kutoka Marekani.

Waziri wa Biashara wa nchi hiyo Mokhethi Shelile ameenda mbele zaidi na kuandaa ujumbe maalumu utakaokwenda nchini Marekani kufanya majadiliano na Rais Trump ya namna ya kulegeza masharti hayo.

Mauzo ya bidhaa Lesotho nchini Marekani yalifika Dola Milioni 237 mwaka 2024.

Mkakati wa Afrika Kusini

Kwa upande wake, Afrika Kusini inafuata mwelekeo tofauti kidogo.

“Wametuwekea ushuru, na sisi tutaangalia madhara ya ushuru huo kwenye uchumi wetu, ndipo tunaweza kuweka wazi msimamo wetu,”alisema Rais Ramaphosa.

Madagascar, ambayo ni kati ya nchi masikini duniani, inakabaliwa na ushuru wa asilimia 47 kwenye bidhaa zake kama vile vanilla na chuma, zenye thamani Dola Milioni 733.

Serikali ya nchi hiyo inafanya majadiliano ya kidiplomasia na Marekani, yenye nia ya kupitia upya ushuru huo.

Maamuzi ya Nigeria

Waziri wa Viwanda wa Nigeria, Jumoke Oduwole, anakiri kuwa ushuru huo utakuwa na athari kubwa kwenye uchumi wa nchi hiyo.

Hata hivyo, kauli ya Oduwole iligusia umuhimu wa kuimarisha biashara ya ndani ya bara la Afrika.

Wito wa kufanya biashara mseto

Uamuzi wa serikali ya Marekani unatoa ukumbusho wa kutokutegemea bidhaa moja ya kuuza nje ya nchi.

Kulingana na wachambuzi, mkakati huu unalenga kujenga ustahimilivu wa kiuchumi wa bara la Afrika.

Maamuzi haya yatakuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa mataifa hayo.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us