Siku ya Jumatatu SADC ilikanusha kuhusika kwake kwa njia yoyote kwa vikosi vyake chini ya SAMIDRC katika operesheni ya kijeshi nchini Congo kama ilivyodaiwa na waasi wa M23 na washirika wake.
SADC ilieleza “wasiwasi wake mkubwa” kuhusu madai hayo yaliyotolewa na waasi hao katika taarifa.
Kundi la M23 na wapiganaji wa AFC walitoa taarifa siku ya Jumamosi iliyodai kuwa vikosi vya SAMIDRC vilihusika katika operesheni ya kijeshi katika mji wa mashariki wa Goma vikishirikiana na wanajeshi wa Congo, na wapiganaji wa FDLR -- kundi lenye silaha huko mashariki mwa Congo -- pamoja na kundi la wapiganaji linalounga mkono serikali la Wazalendo.
“Vikosi vya SAMIDRC havijashiriki katika operesheni yoyote ya pamoja kama inavyodaiwa. Haya madai ni ya kupotosha na hayana msingi,” Taarifa kutoka kwa SADC ilisema.
Jumuiya ya SADC ilisema SAMIDRC inaondoa majeshi yake Congo kwa “utaratibu maalum na kwa makini sana” kwa kuzingatia maamuzi ya mkutano wa SADC, ambayo yalielekeza kumalizika kwa kuwepo kwa vikosi vya SAMIDRC.
Pia walisisitiza msimamo wao kuhusu makubaliano yao na uongozi wa M23 na kuunga mkono juhudi za kuleta amani ya kudumu na utulivu mashariki mwa Congo.
SADC imetoa wito kwa pande zote “kuwa na busara, na kujizuia kueneza taarifa za uongo, na kwa pamoja kushirikiana katika kusitisha mapigano na kurejesha amani katika eneo hilo.”
Tangu mwezi Januari, mashariki mwa Congo imekumbwa na matatizo ya usalama na hali mbaya kwa watu kufuatia mashambulizi mapya ya waasi wa kundi la M23. Waasi hao wanadhibiti maeneo katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
DRC na wengine wanaishtumu nchi jirani ya Rwanda kwa kulisaidia kundi la waasi la M23. Hata hivyo Rwanda, inakanusha madai hayo.
Mwezi Machi, Rais wa DRC Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame walitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika mazungumzo yaliyowashangaza wengi yaliyopatanishwa na kiongozi wa Qatar mjini Doha.