Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia masuala ya haki za binadamu Jumatatu aliangazia kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na vikosi vya RSF huko Kaskazini mwa Darfur, nchini Sudan akisisitiza kushindwa kuwajibika kwa jumuiya ya kimataifa licha ya onyo kutolewa mara kwa mara.
Mashambulizi makali katika kambi za wakimbizi za Zamzam na Abu Shouk, mji wa El Fasher, na eneo la Um Kadada yamesababisha vifo vya mamia ya raia, ikiwemo wafanyakazi wa mashirika ya misaada wasiopungua tisa, Volker Turk alisema katika taarifa.
"Mashambulizi haya yameonesha wazi matokeo ya jumuiya ya kimataifa kushindwa kuchukua hatua, licha ya mimi kuonya mara kwa mara kuhusu hali ya hatari kwa raia katika eneo hilo – ikiwemo Ijumaa iliyopita," Turk alisema.
Machafuko yamesababisha hali ya El Fasher ambayo ni mbaya kuzorota zaidi, eneo ambalo limekabiliwa na mashambulizi ya muda mrefu kutoka kwa wapiganaji wa RSF tangu Mei 2023, alisema.
Pia alieleza wasiwasi wake kuhusu hofu ya machafuko kwa misingi ya kikabila dhidi ya raia ambao wataonekana kuunga mkono Jeshi la Sudan (SAF).
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu aliwakumbusha RSF kuhusu jukumu lao chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu ya kuwalinda raia na kuruhusu waondoke kwa salama katika maeneo ya mapigano.
"Wanaojikuta katikati ya vita wana haki ya kufahamu ukweli, haki na kulipwa fidia," Turk alisema.
Huku mapigano nchini Sudan yakiingia mwaka wake wa tatu sasa, alitoa wito kwa pande zote na zile pande zenye ushawishi juu yao kuchukua hatua madhubuti za kumaliza mzozo huo.
RSF ilianza mashambulizi yake ya hivi karibuni El Fasher Mei 10, 2024, licha ya onyo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu kuzuka tena kwa machafuko katika mji huo,ambao ni sehemu muhimu ya misaada kwa majimbo yote matano yaliyoko Darfur.
Tangu Aprili 15, 2023, RSF imekuwa ikikabiliana na majeshi ya Sudan kwa lengo la kuchukua udhibiti wa nchi, mapigano yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa na chanzo cha kuwa na hali mbaya zaidi kwa watu kuwahi kutokea duniani.