AFRIKA
2 dk kusoma
Shirika la wakimbizi la UN laonya kuhusu 'mzozo juu mzozo' Congo mafuriko yakiwa kero kwa maelfu
UNHCR imetoa wito wa msaada wa dharura huku watu wengi zaidi wakihama makazi yao, na kukiwa na hatari ya magonjwa, pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha
Shirika la wakimbizi la UN laonya kuhusu 'mzozo juu mzozo' Congo mafuriko yakiwa kero kwa maelfu
Raia wakitumia madau katika barabara zenye maji ya mafuriko baada ya mvua kubwa katika eneo la Kinsuka, kaskazini mwa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Januari 10, 2024
15 Aprili 2025

Watu karibu 10,000 wamehama makazi yao katika mkoa wa Tanganyika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa kwa wiki kadhaa, shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia wakimbizi, UNHCR lilisema Jumanne.

"Hali inayojitokeza kwa sasa inaonesha ni mzozo juu ya mzozo kwa DRC, ambapo mafuriko yamezidisha matatizo kwa watu ambao wanakabiliwa na mapigano na kuondolewa katika makazi yao," msemaji Eujin Byun aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva.

Mto Rugumba umefurika, na maji kujaa katika maeneo ya Kalemie na Nyunzu, Byun amesema.

Nyumba, shule na maeneo ya kilimo yameharibiwa, na kuwaacha maelfu bila makazi, alisema, akiongeza kuwa maji yaliyotuwama kutokana na mafuriko yanazua hofu kuhusu mlipuko wa magonjwa, huku maambukizi ya kipindupindu yakiripotiwa katika mkoa huo "ambayo yako mara sita zaidi kama ilivyokuwa kipindi kama hiki mwaka uliyopita."

Tangu Januari, mkoa wa Tanganyika umepokea watu zaidi ya 50,000 waliokimbia kutoka Kivu Kusini. Wengi walikuwa wanapata hifadhi katika majengo ambayo sasa yameharibika.

"Mafuriko pia yameharibu chakula kama mihogo, mahindi, na njugu au karanga, na kutatiza hali mbaya ya ukosefu wa chakula ambayo imekuwepo ndani ya nchi," Byun alisema.

Shirika la UNHCR limeonya kuwa mikoa minne iliyoathirika, ikiwemo Kivu Kusini, Kivu Kaskazini, Ituri, na Tanganyika, watu milioni 2.3 wako kwenye hatari ya kukabiliwa na njaa kali.

Huku shirika hilo na washirika wake wakiendelea kutoa huduma za dharura, "juhudi za kukabiliana na hali yote kwa ujumla zinakwamishwa na ukosefu wa fedha, na kuwaacha maelfu bila msaada wanaouhitaji."

Byun pia alizungumzia kuhusu wakimbizi wanaorejea Congo kutoka Burundi, akisema "hali mbaya za kuishi kwa watu, ikiwemo upatikanaji wa chakula, sehemu ya kuishi na huduma za msingi," licha ya mapigano yanayoendelea.

"Karibu watu 120,000 wamewasili nchini Burundi, Tanzania na Uganda," alisema. "Mtindo huo unaonesha kunahitaka msaada wa haraka kwa nchi wenyeji na maeneo ambayo watu wanarejea."

Kulingana na msemaji huyo, shirika la UNHCR limepokea 20% tu ya fedha inazohitaji kukabiliana na matatizo ya Congo.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us