Mchungaji mmoja wa Marekani mwenye umri wa miaka 45, Josh Sullivan, ameokolewa akiwa salama baada ya ufyatulianaji risasi kati ya maafisa wa usalama wa Afrika Kusini na watekaji wake, polisi walithibitisha siku ya Jumatano.
Sullivan alikuwa ametekwa Alhamisi iliyopita wakati akiongoza ibada katika kanisa lake eneo la Gqeberha, Mkoa wa Cape Mashariki. Watu waliokuwa na silaha walivamia jengo hilo na kumteka, na walikuwa naye kwenye mji huo huo kwa karibu siku tano.
Msemaji wa kitengo cha polisi cha Afrika Kusini cha ‘Hawks’ amethibitisha hilo katika taarifa siku ya Jumatano kuwa Sullivan alipatikana “kwa miujiza bila madhara yoyote” ndani ya gari katika operesheni ya Jumanne usiku, ambapo washukiwa wote watatu wa utekaji waliuawa katika tukio kali la ufyatulianaji risasi.
“Aliyetekwa alipatikana ndani ya gari hilo hilo ambalo washukiwa walikuwa wanafanya mashambulizi kutoka ndani,” Luteni Kanali Avele Fumba alisema.
Wahudumu wa afya walimfanyia tathmini ya haraka Sullivan na yuko katika “hali nzuri,” Fumba amesema.