Sudan Kusini na maajabu ya uhamaji wa Swala
Sudan Kusini na maajabu ya uhamaji wa Swala
Uhamiaji wa swala nchini Sudan Kusini hufanyika kati ya mwezi Januari na Juni ya kila mwaka, ukihusisha swala wenye masikio na aina nyingine ya wanyama hao, ijulikanayo kama 'tiang'.
9 Julai 2025

Najua umezoea kusikia tukio la uhamaji wa mamilioni ya Nyumbu na Pundamilia kila mwaka, kule nchini Tanzania.

Je, unaifahamu ‘The Great Nile Migration’?

Huu ni uhamaji wa makundi ya swala nchini Sudan, ambao hufanyika kati ya mwezi Januari na Juni ya kila mwaka, ukihusisha swala wenye masikio na aina nyingine ya wanyama hao, ijulikanayo kama 'tiang'.

Uhamaji huu, wa aina yake huhusisha makundi makubwa ya swala, ya jamii ya kob, tiang, Mongalla na Bohor, kati Sudan Kusini na kusini-magharibi mwa Ethiopia. 

Wanyama hawa, huhama ukingo wa mashariki wa mto Nile Mweupe kuelekea hifadhi ya taifa ya Boma iliyoko nchini Sudan Kusini, na kuambaa ambaa hadi hifadhi ya taifa ya Gambella nchini Ethiopia. 

Ifikapo mwezi Novemba na Januari, makundi hayo ya mamalia wakubwa hurejea kwenye hifadhi ya taifa ya Boma na Halafu wanarudi kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Boma nchini Sudan Kusini na eneo la Sudd. 

Mbuga hizi mbili za kitaifa za Badingilo na Boma nchini Sudan Kusini ambapo uhamiaji huu hutokea, huhusisha jumla ya hekta milioni tatu ambazo ni makazi ya wanyamapori. 

Swala hao huhama, wakitafuta nyasi fupi fupi zenye virutubisho ambazo hazijaathirika na mafuriko. 

Wakiwa wametulia, swala wenye masikio meupe huishi katika makundi madogo madogo na hutembelea maeneo yale yale ya kulishia na baadaye kuzaliana.

Makundi ya madume hukusanyika pamoja kwa idadi ya swala 15 hadi 20 katika maeneo ya kuzaliana.

Hapo ndipo swala dume huanzisha himaya yake dogo na kushika doria kwenye mipaka dhidi ya washindani.

Kwa upande wao, majike ya swala wakubwa hutembelea eneo hili ili kuchagua madume.

 Hata hivyo, Sudan Kusini haijaweza kuwavutia watalii ili kushuhudia uhamiaji huu.

Hii ni kutokana na ukosefu wa utulivu nchini humo tangu nchi hiyo kupata uhuru mwaka 2011, huku vita vya wenyewe kwa wenyewe, vikifanya vivutio vingi vya asili kutokuwa salama kwa watalii. 

Kwa sasa serikali ya nchi hiyo ambayo ni changa zaidi duniani inajitahidi kurejesha amani ya kudumu baada ya makubaliano ya awali ya mwaka 2018.

Na iwapo amani na usalama utapatikana, basi wataalamu wanasema, Sudan Kusini huenda ikawa ni moja ya vivutio vikubwa vya watalii barani Afrika.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us