Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Burhanettin Duran ameteuliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Mawasiliano wa Uturuki, kwa mujibu wa amri ya Rais iliyochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali mapema Alhamisi.
Anachukua nafasi ya Fahrettin Altun, ambaye alishikilia wadhifa huo tangu Julai 25, 2018, na sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu na Usawa la Uturuki (TİHEK).
Duran ana shahada katika Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Bogazici na shahada ya uzamivu katika Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Bilkent.
Hapo awali aliwahi kuwa mratibu mkuu wa Wakfu wa SETA na aliteuliwa katika Baraza la Usalama wa Rais na Sera za Kigeni mnamo 2018.
Alikua Naibu Waziri wa Mambo ya Nje mnamo Mei 2024.
Altun alithibitisha kuondoka kwake kutoka wadhifa huo na kutangaza uteuzi mpya kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii, akitoa shukrani kwa Rais Recep Tayyip Erdogan kwa kuwa na imani naye na msaada wa Rais katika kipindi cha miaka saba alichohudumia katika wadhifa wake.
“Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Rais aliyenikabidhi nafasi hii, kwa familia yangu, kwa wafanyakazi wenzangu ambao walifanya kazi bila kuchoka katika Muundo wa Mawasiliano wa Uturuki, na kwa wanahabari wote waliosimama kidete katika kupigania ukweli,” aliandika.
Pia alimtakia heri Duran, akimtaja kama "rafiki na ndugu wa thamani" ambaye alifanya naye kazi kwa karibu kwa miaka mingi.