Kadhi Mkuu wa Kenya, Sheikh Athman Abdulhalim Hussein, amefariki dunia leo, Alhamisi Julai 10, 2025, akiwa mjini Mombasa.
Taarifa za kifo chake zimetolewa na Imamu wa Msikiti wa Jamia, Sheikh Jamaludin Osman ambapo amesema kuwa mazishi yake yatafanyika leo baada ya swala ya alasiri, mjini Mombasa, Kenya.
Sheikh Abdulhalim aliteuliwa kuwa Kadhi Mkuu Julai 17, 2023, na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), amechukua nafasi ya Sheikh Ahmed Muhdhar aliyestaafu Disemba 2022. Na kuwa Kadhi Mkuu wa 12 nchini Kenya.
Kabla ya kuteuliwa kwake, alikuwa akihudumu kama Kadhi Mkuu Msaidizi wa Nairobi, na pia aliwahi kuhudumu katika maeneo ya Kwale, Mombasa na Isiolo.
Alisomea Sheria za Kiislamu katika Chuo Kikuu maarufu cha Al-Azhar nchini Misri, na alipata mafunzo maalum ya mahakama nchini Saudi Arabia.
Uteuzi wake ulitokana na uzoefu wake mkubwa na dhamira yake ya kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu nchini Kenya.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Sheikh Abdulhalim alisisitiza mshikamano wa Waislamu, hususan katika masuala ya kuandama kwa mwezi kwa pamoja ili kuepusha mgawanyiko wakati wa Ramadhani na Sikukuu za Eid.
Alianzisha pia mikakati ya kuharakisha huduma katika mahakama za Kadhi.
Sheikh Abdulhadlim aliamini kuwa ofisi ya Kadhi Mkuu haipaswi kuwa ya mtu mmoja au kundi moja, bali iwe jukwaa la ushirikiano na wasomi wengine wa Kiislamu na vyombo vya haki nchini.