Miongo mitatu tangu uhuru wa Afrika Kusini sasa Wazungu walioko huko wajulikanao kama Afrikaans wanadai kujitenga kuunda nchi yao isiyo na Wa-Afrika weusi. Na ndio wanayoita Orania.
Wazungu hao wa Afrikaans walipinga utawala wa watu weusi walio wengi wakati wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid ulipomalizika takriban miongo mitatu iliyopita hivi kwamba walichonga eneo la watu wanaotaka kujitenga, mji pekee nchini Afrika Kusini ambapo wakaazi wote, wakiwemo wafanyakazi za mikono ni wazungu.
Sasa, wakaazi wa Orania - idadi ya watu, 3,000 - katika eneo lenye ukame la Karoo wanamtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuwasaidia kujitenga na kuwa taifa huru.
Wiki iliyopita, viongozi wa jamii kutoka Orania waliitembelea Marekani kutafuta kutambuliwa kama chombo kinachojiendesha. Mamlaka za Afrika Kusini zinaukubali kama mji ambao unaweza kuongeza ushuru wa ndani na kutoa huduma.
Kumbukumbu za viongozi wa apartheid
Viongozi wa Orania wamesema kuwa wanataka kutumia fursa hii ambapo Marekani imeimulika Afrika Kusini kutafuta kuungwa mkono na utawala wa Trump kuweza kujitenga.
"Tulitaka... kupata kutambuliwa, huku Marekani ikilenga Afrika Kusini sasa," kiongozi wa Orania Movement Joost Strydom aliiambia Reuters.
Wenyeji waliounda mji huo wameupamba kwa masanamu ya shaba ya viongozi wa zamani wa Afrikaner, ikiwa ni pamoja na wale wa tangu enzi ya utawala wa kibaguzi wa Apartheid ambao ulikomeshwa na upinzani wa ndani na hasira ya kimataifa.
Makazi hayo ya hekta 8,000 yamepata wimbi kubwa la uungwaji mkono kutoka kwa Wamarekani wa mrengo wa kulia kwa wazalendo wa Kiafrikaner, ambao walipoteza mamlaka yao yote wakati ubaguzi wa rangi ulipoisha mwaka 1994 na Nelson Mandela kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.
Taifa lenye mchanganyiko wa watu
Huko New York na Washington viongozi wa Orania walikutana na watu wenye ushawishi, waunda sera na wanasiasa wa ngazi za chini wa Republican.
"Tuliwaambia Afrika Kusini ni nchi yenye mchanganyiko mbali mbali wa watu na kwamba sio wazo zuri kujaribu kuisimamia serikali kuu kutoka sehemu moja," alisema Strydom.
Lakini walipohojiwa juu ya ajenda yao, walisema kuwa hawataki misaada kutoka Marekani bali wanataka utambulisho na uekezaji wa hali ya juu utakaowasaidia kujenga mji wao wanaobashiri kukuwa kwa kasi ya asili mia 15 kwa mwaka.
Hata hivyo walikataa kujibu iwapo walikutana na maafisa wowote wa ofisi ya Trump.
Orania sio nchi!
Serikali ya Afrika Kusini imepuuza juhudi zao hizi ikisema kuwa yeyote anayeishi katika ardhi ya Afrika Kusini yupo chini ya sheria ya taifa la Afrika Kusini.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini Chrispin Phiri aliiambia Reuters: " Orania si... nchi. Wako chini ya sheria za Afrika Kusini na ... katiba yetu."
Lakini msimamo wa Trump tangu kutokea tofauti kati yake na serikali ya Afrika Kusini ni kuwa Wazungu wote walioko Afrika Kusini wahamie Marekani na atawapa eneo la kulima. Ofa ambayo wameipuuza na kusema kuwa hawataki kuondoka katika ardhi yao.
Makundi mengine ya wafuasi wa Afrikaan pia yametembelea Marekani ili kujenga ushirikiano na washirika wengi weupe, wa chama cha Republican, na kuibua shutuma nyumbani kwamba safari kama hizo zilizua migawanyiko ya rangi.
Tishio kwa umoja wa kitaifa
Chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF) mapema mwezi Aprili kiliwashutumu viongozi wa Orania kwa "kuharibu umoja wa nchi hii", shutuma ambayo imekanushwa.
Afrikaan ni kabila la wazungu kutoka Uholanzi waliohamia Afrika Kusini miaka ya 1600. Walipinga utawala wa kikoloni wa Waingereza japo waliposhinda walishika wao usukani wa ukoloni wa Afrika Kusini na kuwabagua watu weusi asili wa nchi hiyo.
"Kulikuwa na sheria 17,000 kuhusu ardhi pekee," Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Phiri alisema. "Tulilazimika... kujenga upya Afrika Kusini kuwa nchi ambayo inawakilisha wale wote wanaoishi humo."
Mnamo mwaka wa 1991, mwisho wa ubaguzi wa rangi ulipokaribia, kikundi cha kabila la Afrikaan wapatao 300 kilinunua eneo la Orania, mradi wa maji ulioachwa hapo awali kwenye Mto Orange wenye tope, ili kuunda nchi ya Waafrika Wazungu pekee.
Tamaa ya uhuru
"Ni mwanzo wa kitu," kiongozi wa zamani wa Harakati ya Orania Carel Boshoff, alisema kuhusu jamii yake, akilinganisha tamaa yake ya uhuru - Orania hata hutumia sarafu yake isiyo rasmi - na ile ya Israeli, iliyoanzishwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia licha ya upinzani mkali kutoka kwa Waarabu wanaoishi katika eneo hilo.
Boshoff, ambaye baba yake alianzisha mji huo na babu yake, Hendrick Verwoerd, anatazamwa sana kama mbunifu wa ubaguzi wa rangi, ana ndoto za eneo linaloenea hadi pwani ya magharibi karibu maili 1,000.
Shughuli za Orania hufadhiliwa kupitia ushuru wa ndani na michango kutoka kwa wafuasi na wakaazi.
Japo kwa sasa bado wanaonekana tu kuwa wazo lisilo tishio kwa serikali ya Afrika Kusini, wachambuzi wanaonya kuwa huenda ni chimbuko la vuguvugu litakaloiletea Afrika Kuisni kero ya utengano na ubaguzi wa rangi katika siku zijazo.