Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamekubaliana kwa pamoja kuchukua hatua za dharura kutatua mgogoro wa Sudan, huku wakizitaka pande zinazozozana kuchukua hatua za haraka kuheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa.
Katika taarifa ya pamoja kufuatia mkutano wa London wa Jumanne, viongozi hao wametilia mkazo msimamo wao kwa uhuru, umoja na kuheshimu mipaka ya Sudan.
“Tunatambua dharura ya hali ya kibinadamu and tumejadiliana jinsi gani tunaweza kuimarisha jitihada za kufikisha msaada kwa wale wanaohitaji zaidi,” wamesema.
Taarifa hiyo imekuja baada ya Mkutano wa siku moja wa London kwa kushirikiana na Uingereza, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, ambapo mawaziri wa mambo ya nje na viongozi wa masuala ya kibinadamu walikusanyika katika mwaka wa pili tangu kuanza kwa mgogoro huo.
Uwakilishi wa dunia
Wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka nchi kama vile Canada, Misri, Ethiopia, Kenya, Saudi Arabia, Norway, Qatar, Uturuki na Marekani walikuwa ni miongoni mwa waliohudhuria, pamoja na mawaziri wa mambo ya nje kutoka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, pamoja na Kamishna wa Masuala ya Migogoro Ulaya Hadja Lahbib na Bankole Adeoye, kamishna wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Siasa, Amani na Ulinzi.
Taarifa hiyo imegusia kwamba mgogoro wa Sudan unaingia katika mwaka wake wa tatu huku raia wa nchi hiyo wakiendelea kukabiliwa na hali mbaya na mateso.
“Kipaombele ni kufikia usitishwaji wa mapigano haraka na kumaliza mgogoro,” imesema sehemu ya taarifa, na kuongeza kwamba washiriki wamekataa vitendo vyote, ikiwemo ushawishi wa nje, ambao unaongeza hali ya wasiwasi au kurefusha mapigano.
Wakielezea kuunga mkono hali ya mpito kuelekea serikali ya kiraia nchini Sudan, wamesema kwamba ni lazima raia wa Sudan waamue mustkabali wa kisiasa wa nchi yao.
‘Hatua ya haraka
“Kutambua dharura ya mgogoro wa hali ya kibinadamu…washiriki wamesisitiza wito wao kwa pande zinazopigana kuchukua hatua za haraka kuheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa, na kuwatoa raia wa Sudan kutoka katika mateso,” wamesema.
Pia wamezitaka pande zote kuhakikisha usalama wa raia, na kuwezesha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu.
Tangu Aprili 15, 2023, vikosi vya RSF vimekuwa vikipigana na jeshi ili kuchukua mamlaka ya nchi, na kusababisha vifo vya maelfu na moja ya mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu kuwahi kutokea duniani.